CHANZO: Urban Pulse na Freddy Macha
Jumapili mchana  wilaya ya Westminster jijini  London ilikuwa na mashindano ya ubunifu na
urembo katika maonyesho  ya kimataifa ya London
Fashion Week. Mashindano haya yalifanyika jumba la Somerset lililosimama
imara  kwenye upembe wa  kaskazi ya mto Thames.
Maonyesho ya London Fashion Week, bado yanaendelea jumba
hili  la Somerset toka tarehe 14 hadi
tarehe 28. Wiki hizi mbili nzima zitakutanisha kila mtu anaye husika na
biashara ya mavazi na urembo. Magwiji na mapapa wa mitindo, wabunifu,
walimbwende, watafuta vipaji, wafanya biashara, wazalishaji mali ghafi na
wamiliki viwanda.  Wote hukutana katika
maonyesho haya. Hapa si vipaji tu vinavyojionyesha, bali pia watu wa biashara.
Siku hii Tanzania ilikuwa moja ya nchi mbili tu za Kiafrika
zilizochaguliwa na British Council na LFW kushiriki kwenye mashindano  ya kutafuta vipaji chipukizi kwenye tasnia ya
ubunifu wa mavazi na urembo.  Watanzania
Anna Lukindo, Jacqueline Kibacha na 
Christine Mhando ndio wasanii waliobeba bendera ya taifa letu na
kutuwakilisha katika mashindano haya ya kimataifa yanayofanyika kila mwaka kwa
zaidi ya miaka 27 sasa.
Katika kuunga mkono maendeleo ya Tanzania na
Watanzania,  Ubalozi wetu  Uingereza na Bodi ya Utalii Tanzania, nao pia
walichukua nafasi hii kuwasaidia wananchi hawa kufanikisha mahitaji yao ya
ushindani. Ubalozi umetoa Ukumbi wa Nyumba Ya Tanzania ulioko Bond Street ili
wasanii hao waweze kuonyesha nguo na sanaa zao kwa juma zima kama sheria za
London Fashion Week zinavyoamuru. Vile vile Bodi ya Utalii ya Tanzania imesaidia
katika mchango  wa mali ghafi
zilizotumika katika shughuli hizi  ili
kuiuza Tanzania kimataifa.
Mshindi wa tukio alikua Estonia. Ingawa  Tanzania haikuwa mshindi wa mwanzo-
ilichaguliwa kati ya Kumi Bora jambo ambalo limetikisa nyoyo na vichwa vya  waandaaji, wabunifu,wafanya biashara na
watafuta vipaji vya kimataifa. Hii ni mara ya kwanza kwa taifa letu kushiriki
katika shughuli na  wote wameguswa na
kupumbazwa na usanii wa hali ya juu ulioonyeshwa na wasanii  watatu wa Kitanzania.   Lukindo, Mhando na Kibacha wamechukua nafasi
waliyopewa kwa mikono miwili na wote wameisogeza Tanzania hatua moja zaidi
ndani ya ulingo wa kimataifa na katika biashara hii ya mavazi na urembo ambayo
inasemekana ina thamani ya  Pauni Billioni
10  ama 
shilingi Trillion 25 za Tanzania.



EmoticonEmoticon