REPIN ROCK CITY

REPIN ROCK CITY

TUMA TRACK YAKO

FAGIO LA MWAKYEMBE: 11 KIKAANGONI TPA TANGA

11:51:00 PM Add Comment


FAGIO la Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe la kusafisha uozo katika Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) sasa limehamia katika Bandari ya Tanga ambapo jumla ya wafanyakazi 11 wamepewa barua za kujieleza walivitoa wapi vyeti walivyowasilisha kwa mwajiri wao.

Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na Meneja TPA Tanga, Awadhi Massawe  zilisema wafanyakazi hao ni wale waliopata ajira mpya  Septemba mwaka jana na hatua ya kuwaandikia barua imefikiwa baada ya kuwasiliana na Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA) .

Wafanyakazi hao ni wa Idara za Operesheni, Marine na Ulinzi ambao waliajiriwa  mwaka jana baada ya nafasi zao kutangazwa na kufanyiwa usaili.

Wafanyakazi hao waliopewa barua za kujieleza ni 11 kati ya waliofuzu usaili uliosimamiwa na maofisa wa TPA Tanga na baadaye  kuonekana kufanya vizuri kuwashinda waombaji wengine.

“Hapa bandarini sasa hivi hakuna raha kila mtu ana wasiwasi, hawa  vijana walishaajiriwa na kulipwa mishahara, lakini leo wanaambiwa kuwa hawafai, imetushtua sana,”alisema mfanyakazi aliyejitambulisha kwa jina moja la Mariam.

Ilielezwa kuwa barua za kuwataka watoe maelezo ya vyeti vyao zilianza kusambazwa Jumatatu wiki iliyopita na kwamba hivi sasa baadhi yao hawafiki tena kazini kutokana na kuhofia kukamatwa.

Akithibitisha habari hizi, Massawe alisema ni kweli kuna watumishi 11  waliopewa barua za kujieleza juu ya vyeti vya kuhitimu kidato cha nne na sita, lakini bado hawajafukuzwa kazi.

Meneja huyo alisema katika kipindi cha kukamilisha mkataba wa waajiriwa hao, TPA iliwasilisha vyeti vyao kwenye NECTA ili kujua kama ni halali au la, ndipo ikabainika hao 11 vyeti  vyao havikutoka NECTA.

Alisisitiza kuwa wakati wa ubabaishaji katika kutoa ajira TPA sasa umekwisha ili kuleta ufanisi.
 sheria ili kuleta ufanisi na kuondoa malalamiko ambayo yamekuwa  yakijitokeza mara kwa mara.

“Baada ya NECTA kuvikana  vyeti vya waajiriwa hao wapya, polisi wameanza kufanya uchunguzi ili kuwafikisha mahakamani kwa kughushi vyeti,” alisema.

Inasemekana vyeti hivyo vyote bandia vimetengezwa sehemu moja iliyopo jijini Dar es salaam na kwamba ilibainika hivyo baada ya mmoja wa  wafanyakazi hao kubanwa na kuwataja wengine kuwa wote wamechapishiwa na mtu mmoja.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga,Constantine Massawe hakutaka kuelezea juu ya sakata hilo na kusisitiza kuwa atazungumza na  vyombo vya habari mara uchunguzi utakapokamilika.

MWANANCHI

TAARIFA: RUSHWA KUITAFUNA JWTZ

11:36:00 PM Add Comment


TANZANIA imetajwa kuwa ni miongoni mwa nchi zinazokabiliwa na tatizo la rushwa ndani ya jeshi.Taasisi ya Transparency International (TI), ambayo hutafiti masuala ya rushwa duniani imeitaja Tanzania kwamba jeshi lake lina rushwa kubwa na ndogondogo.

Kwa mujibu wa gazeti dada la The Citizen la jana Jumapili, uongozi wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) umekanusha vikali taarifa ya taasisi hiyo.

TI inadai katika taarifa yake kuwa sekta ya ulinzi ya Tanzania inakabiliwa na tatizo hilo na hiyo ni kutokana na mambo yake kuendeshwa kwa usiri mkubwa.

“Hakuna kitu kibaya kama la rushwa kwenye jeshi, maana kuna fedha nyingi inatembea kutokana na ughali wa vifaa vya kijeshi. Bado Serikali nyingi zinafanya mambo haya kuwa siri na kutoa mwanya kwa rushwa kutembea.
“Fedha inayotumika vibaya kwa masuala ya kijeshi, ingeweza kutumia vizuri zaidi katika masuala ya maendeleo,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo iliyoandikwa na Mark Pyman, ambaye ni Mkurugenzi wa Kitengo cha masuala ya Ulinzi cha Transperancy International.

Transparency International inaeleza kuwa fedha ya rushwa inayotembea kwenye sekta ya ulinzi inakadiriwa kufikia kiasi cha Dola 20 bilioni (Sh32 trilioni).

“Ripoti ya Transparency International itufungue macho Watanzania maana kwa kawaida huwa kila watu wakihoji mapato na matumizi ya jeshi tunaambiwa hatuwezi kujibiwa kwa madai ya woga wa kuhatarisha usalama wa taifa,” alikaririwa mbunge mmoja na gazeti la The Citizen.

Tanzania, hata hivyo, iko juu ya nchi nyingi za Afrika kwa tatizo la rushwa ingawa inatakiwa kurekebisha mianya mingi kwenye sekta hiyo.

“Tunaona Tanzania ina changamoto ya kuimarisha vyombo vya kutupa jicho kwenye jeshi. Mathalani, kuna Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Mambo ya Nje, lakini haina meno ya kuingia kwa undani masuala ya kijeshi,” iliongeza Transparency International.
Msemaji wa JWTZ, Kanali Kapambala Mgawe, hata hivyo, alikaririwa na gazeti la The Citizen akidai kuwa taasisi yake imekuwa ikifanya kazi kitaalamu na kimaadili akitolea mfano jinsi wanavyoajiri wanajeshi kwa kufuata vigezo.

Transparency International inasema kuwa kuna Kitengo cha Utawala Bora cha Serikali ambacho hufanya ukaguzi kwenye jeshi ingawa halijatoa ripoti ya aina yoyote kuhusiana na ukaguzi wa bajeti ya jeshi. “Mfano kuna taarifa kuwa Kitengo cha Kilimo cha Jeshi la Kujenga Taifa (Suma-JKT) kuna kinajishughulisha na uchimbaji madini na biashara nyingine lakini kuna udhibiti mdogo,” iliongeza taarifa yao.

Julai mwaka jana, maofisa saba waandamizi wa Bodi ya Zabuni ya Suma-JKT walifunguliwa mashitaka ya matumizi mabaya ya ofisi na uhamishaji usio wa halali wa zaidi ya Sh 3.8 bilioni.
Waliotuhumiwa ni pamoja na Kanali Ayoub Mwakang’ata, Luteni Kanali Mkohi Kichogo, Luteni Kanali Paul Mayavi, Meja Peter Lushika, Sajini John Laizer, Meja Yohana Nyuchi na Luteni Kanali Felix Samillan wanaodaiwa kufanya makosa hayo mwaka 2009.

Tanzania imewekwa katika Kundi D kwenye orodha hiyo ya Transperancy International ya nchi zinazokabiliwa na kiwango cha juu cha rushwa na vigezo vinavyoangaliwa ni sekta za siasa, fedha, utumishi wa Kundi la D ni nchi ambazo zinakabiliwa na kiwango cha juu cha rushwa na katika orodha hiyo zimo pia nchi za Russia na China.

Hata hivyo, nchi zenye kiwango cha juu cha rushwa ziko katika Kundi F wakati zile zenye kiwango cha chini cha rushwa ziko Kundi A.

MWANANCHI

IKULU: RAIS KIKWETE KUHUDHURIA MAZISHI YA BABA WA RAIS MUSEVENI

11:25:00 PM Add Comment


AHSANTENI SANA KWA UKARIMU WENU : Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiagana na  maafisa mbalimbali wa ubalozi wa Tanzania Nchini Ethiopia katika Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Bole jijini Addis Ababa jana jioni ya Februari 24, 2013 baada ya kuhudhuria hafla ya Utiaji saini Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Amani, Usalama na Ushirikiano katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Rais Kikwete, kabla ya kurejea Dar es salaam leo, alikwenda Uganda kuhudhuria mazishi ya baba mzazi wa Rais Yoweri Kaguta Museveni, Mzee Amos Kaguta, aliyefariki siku ya Ijumaa na kuzikwa kijijini kwake


KWA HERI MHESHIMIWA..KARIBU TENA : Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia Profesa Joram M. Biswaro akiwa na Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda Balozi Naimi Aziz (kati) na Afisa ubalozi Samwel Shelukindo wakipungia kumuaga Rais Kikwete wakati ndege yake ikiondoka uwanjani hapo leo jioni ya  Februari 24, 2013.

Picha na IKULU

AFYA: MUHIMBILI NA AGA KHAN KUTOA HUDUMA YA UPASUAJI WA MOYO

11:17:00 PM Add Comment


HUDUMA za matibabu na upasuaji wa moyo zitaanza kupatikana nchini, kutokana na mipango ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na ile ya Aga Khan.

Hatua hiyo itawawezesha wagonjwa wa moyo nchini kutopelekwa kwa wingi nje ya nchi kama ilivyo sasa. Pia itaokoa mamilioni ya fedha ambazo zimekuwa zikitumika kugharimia tiba hiyo nje ya nchi.

Mkurugenzi wa Huduma za Afya wa Hospitali za Aga Khan Tanzania, Dk Jaffer Dharsee akiwasilisha taarifa kuhusu ongezeko la magonjwa ya moyo nchini katika kongamano la wataalamu wa magonjwa hayo alisema, jitihada kubwa zinafanywa ili kuhakikisha tiba ya moyo inaanza kutolewa nchini.

Alisema Hospitali ya Muhimbili inakusudia kuanza kutoa tiba hiyo katika kipindi cha miezi miwili ijayo baada ya ujenzi wa taasisi yake kukamilika, wakati Hospitali ya Aga Khan itaanza kutoa matibabu hayo mwakani. Kongamano hilo lilifanyika mwishoni mwa wiki iliyopita jijini Dar es Salaam.

Hatua ya kuwapo kwa tiba za moyo nchini, itawezesha gharama za tiba kupungua kwa asilimia 57.1, ikilinganishwa na gharama za tiba hizo nje ya nchi.

Dk Dharsee alisema hapa nchini gharama za tiba zitakuwa Dola za Marekani 1,500 sawa na Sh2.4 milioni tofauti na Dola 3,500 (Sh5.6 milioni) zinazotumika kumpeleka mgonjwa kwa ajili ya upasuaji nchi za nje kama India.

Alisema gharama hiyo inatokana na kuwapo kwa gharama kubwa zinazohitajika kuandaa maabara hiyo ambayo ina thamani ya Dola 200 milioni (Sh320 bilioni) bila kuingiza gharama za wataalamu wa kuiendesha na kuhudumia wagonjwa.

SAKATA LA MATOKEO YA MTIHANI WA KIDATO CHA NNE: MTIHANI ULIKUWA KATIKA MFUMO TOFAUTI

11:09:00 PM Add Comment


Na Fredy Azzah na Kelvin Matandiko 
MATOKEO mabaya ya mtihani wa kidato cha nne yamezidi kuibua mapya, baada ya wamiliki wa shule na vyuo binafsi nchini kusema mitihani ilitungwa kwa mfumo tofauti na uliozoeleka miaka yote, huku tume iliyounndwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ikipondwa na baadhi ya watu.Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi nchini (TAMONGSCO), Mahmoud Mringo alisema kwamba maswali waliyoulizwa watahiniwa yalikuwa ya kujieleza tofauti na miaka ya nyuma, ambapo
mfumo uliotumika uliwataka watahiniwa kutaja vitu tu bila ya kulazimika kuvielezea kwa undani.

Kauli yake iliungwa mkono na Mkuu wa Taaluma katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Marian, Florence Mapunda ambaye alisema kuwa mtihani wa mwaka jana ulitaka zaidi watoto kujieleza tofauti na 
miaka ya nyuma wakati wanafunzi walipokuwa wanakariri.

Hata hivyo, Msemaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), John Nchimbi alisema mfumo wa mtihani haukubadilika kwa namna yoyote na kuwa upo kama ule wa miaka yote.

Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philip Mulugo, kwa upande wake alisema madai yanayotolewa hayana msingi, huku akihoji kwa nini yasitoke tangu mitihani ilipokuwa ikifanyika na badala yake yanatoka baada ya kutangazwa kwa matokeo.

Matokeo ya mtihani wa kidato cha nne uliofanyika mwaka jana yanaonyesha kuwa watahiniwa 240,903 sawa na asilimia 60.6 wamepata sifuri, huku wanafunzi 23,520 tu ambao ni sawa na asilimia 5.16 ndiyo waliofaulu na wengine 103,327 sawa na asilimia 26.02 wamepata daraja la nne.
Kutokana na matokeo hayo, Waziri Mkuu Pinda, juzi alitangaza kuunda tume ya kuchunguza chanzo cha matokeo hayo kuwa mabaya, hatua ambayo hata hivyo imekosolewa na wasomi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Tume hiyo inayoundwa na wajumbe kutoka Taasisi za Elimu, Chama cha Waalimu, Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii na Umoja wa Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (Tahossa) inatarajiwa kuanza kazi wiki hii.

Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema kuunda tume ni kupoteza muda kwa sababu matatizo na changamoto zote ndani ya sekta hiyo yanajulikana, huku mwenzake, Profesa Chriss Maina pia wa UDSM akisema kuunda tume hakutaisaidia kwa kuwa Serikali inaidharau sekta ya elimu.
“Tatizo ni kutowekeza kikamilifu katika sekta ya elimu, imekuwa na matumizi makubwa katika mambo yasiyokuwa ya lazima,”alisema Profesa Mpangala.

Alisema matatizo mengine ni mazingira magumu ya kufundisha na uhaba wa walimu. “Kinachotakiwa wajipange kufanyia kazi changamoto hizi zilizopo badala ya kuunda tume, wakati fedha nyingi tunasikia inapotea kwenye ubadhirifu,”alisema Profesa Mpangala.

Naye Profesa Maina alisema: “Hiyo tume ya kazi gani kwa sababu matatizo yanafahamika wazi, umewahi kusikia taifa gani ambalo halina mtalaa wa elimu. Hiyo ndiyo hali halisi kwa nchi yetu. ”

MNADA BANNER