1. Jeshi la Polisi Nchini, linawakumbusha wananchi wote
kuwa, tunapoelekea kipindi hiki cha sikukuu za Christmas na Mwaka Mpya
itakayoadhimishwa kati ya tarehe 24-26 Disemba, 2012 na tarehe 01 Januari, 2013
wanatakiwa kusherehekea sikukuu hizo kwa amani na utulivu pasipo vitendo ama
viashiria vyovyote vya uvunjifu wa sheria. Wananchi wote wachukue tahadhali kwa
kushirikiana na Jeshi la Polisi kuhakikisha kuwa vitendo vyote vya uhalifu na
wahalifu kwenye maeneo mbalimbali vinadhibitiwa.
2. Ikumbukwe kuwa, wananchi wenye imani ya Kikristo na hata
madhehebu mengine hutumia muda huo kwenda kuabudu pamoja na muendelezo wa
sherehe hizo kwenye maeneo mbalimbali ya starehe, uzoefu unaonyesha kuwa baadhi
ya watu hutumia kipindi hicho cha sikukuu kufanya matukio ya uhalifu kutokana
na mikusanyiko hiyo ya watu.
3. Jeshi la Polisi limejipanga kikamilifu kuhakikisha kwamba
wananchi kote nchini wanasherekea sikukuu hizo kwa amani na utulivu, ulinzi
umeimarishwa kwenye maeneo yote ya kuabudia, fukwe za bahari, sehemu za starehe
na maeneo mengine yote ambayo yatakuwa na mikusanyiko mikubwa ya watu.
4. Aidha, tunawatahadharisha wale wote ambao watakuwa
wakitumia barabara, kuwa makini kwa kuzingatia sheria za usalama barabarani,
madereva kuepuka kwenda mwendo kasi na kutumia vilevi wawapo kazini.
5. Katika kuhakikisha usalama kwenye kumbi za starehe,
wamiliki wa kumbi hizo wazingatie uhalali na matumizi ya kumbi zao katika
uingizaji wa watu kulingana na uwezo wa kumbi hizo, badala ya kuendekeza tamaa
ya fedha kwa kujaza watu kupita kiasi. Vilevile, wazazi wawe makini na watoto
wao na hasa disko toto na kutokuwaacha kutembea peke yao, ili kuepuka ajali na
matukio mengine yanayoweza kusababisha madhara juu ya watoto hao.
6. Wananchi wote wanakumbushwa kwamba, watokapo kwenye
makazi yao wasiache nyumba wazi ama bila mtu na endapo kuna ulazima wa kufanya
hivyo watoe taarifa kwa majirani zao, na pale wanapowatilia mashaka watu
wasiowafahamu wasikae kimya bali watoe taarifa kwa Jeshi la Polisi ili hatua
stahiki ziweze kuchukuliwa haraka kwa wahusika kupitia namba simu 0754 785557
ama namba za viongozi wa polisi zilizokwishatolewa hapo awali.
7. Jeshi la Polisi linatoa wito kwa taasisi mbalimbali za
serikali, madhehebu ya dini, asasi za kiraia, vyama vya siasa, vyombo vya
habari, makampuni binafsi ya ulinzi na wananchi kwa ujumla, kuendelea kutoa
ushirikiano na hasa katika kipindi cha mwisho wa mwaka, ili kuhakikisha usalama
wa nchi yetu unadumishwa na raia wote wema wanaishi kwa amani na utulivu bila
hofu ya uhalifu.
8. Mwisho, nawahakikishia wananchi kwamba, Jeshi la Polisi
linatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria za nchi na hivyo
halitawajibika kumwonea huruma ama upendeleo mtu yeyote atakayeenda kinyume na
sheria.
NAWATAKIENI WATANZANIA WOTE KHERI YA CHRISTMAS NA MWAKA
MPYA.
Advera Senso-ASP
Msemaji wa Jeshi la Polisi (T)
POLISI MAKAO MAKUU.
EmoticonEmoticon