Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella
Mukangara (wa tatu kulia)
akiangalia jana nyavu za kuvulia samaki
za Kikundi cha Msifuni kilichopo katika kijiji cha Kemondo wilayani Bukoba
ambacho kilipata mkopo kutoka mfuko wa maendeleo ya vijana na kuanzisha mradi
wa bwawa la samaki. Kushoto ni Katibu wa kikundi hicho Johanes Joel.
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella
Mukangara (kushoto) akiangalia kahawa
iliyolimwa na Ibrahim Mulokozi (kulia) ambaye ni mkazi wa kijiji cha Ibwera
wilayani Bukoba aliyenufaika na mkopo wa shilingi laki nne kutoka mfuko wa
maendeleo ya vijana. Waziri Dk. Mukangara alilitembelea shamba hilo la kahawa
na migomba jana ili kuona fedha za mkopo walizozipata vijana kutoka SACCOS ya
Ibwera zimewanufaishaje kimaisha.
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella
Mukangara (kushoto) akimuangalia samaki
mwenye umri wa miezi mitatu anayefugwa katika bwawa la Kikundi cha Msifuni
kilichopo kijiji cha Kemondo wilayani Bukoba ambacho kilipata mkopo kutoka
mfuko wa maendeleo ya vijana. Waziri Dk. Mukangara alilitembelea bwawa hilo jana
ili kuona fedha za mkopo walizozipata vijana kupitia mfuko wa Halmashauri
nimewasaidiaje vijana kujikwamua kiuchumi.
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella
Mukangara (kushoto) akipokea taarifa ya
SACCOS ya Ibwera iliyopo wilayani Bukoba
kutoka kwa Benedicta Peter ambaye ni katibu msaidizi. SACCOS hiyo ilipata mkopo wa shilingi milioni tano kutoka
mfuko wa maendeleo ya vijana.
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella
Mukangara (wanne kushoto) akiwa katika
picha ya pamoja na wanachama wa SACCOS ya Ibwera na viongozi wa wilaya ya
Bukoba wakati alipowatembelea jana ili
kuona fedha walizopata kutoka mfuko wa waendeleo ya vijana zilivyoweza kuwasaidia vijana kujikwamua
kimaisha. (Picha na Anna Nkinda – Maelezo).
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella
Mukangara akiangalia shamba la kahawa na
migomba la mkazi wa kijiji cha Ibwera wilayani Bukoba Ibrahim Mulokozi (haupo
pichani) wakati alipolitembelea jana ili
kuona fedha za mkopo wa mfuko wa vijana alizozipata kupitia SACCOS ya Ibwera
zimemnufaishaje kimaisha. Kushoto ni
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Maendeleo ya Vijana James Kajugusi.
Na Habari Maelezo, Kagera
Serikali imeombwa
kuongeza kiasi cha mkopo kinachotoa kwa vijana kupitia mfuko wa maendeleo wa
vijana na Halmashauri za wilaya kwani kiwango kinachotolewa kwa sasa cha
shilingi milioni tano kwa vyama vya Kuweka Akiba na Kukopa (SACCOS) ni kidogo
ukilinganisha na mahitaji ya mkopo huo.
Ombi hilo limetolewa jana na baadhi ya vijana waliopata mkopo huo kupitia SACCOS ya
Ibwera na halmashauri ya wilaya ya Bukoba wakati wakiongea kwa nyakati tofauti
na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella Mukangara alipotembelea wilaya hiyo ili kuona jinsi
fedha hizo zilivyoweza kuwasaidia vijana kujikwamua kiuchumi.
Vijana hao walisema kuwa fedha za mkopo walizozipata
zimewasaidia kujiinua kiuchumi ikiwa ni pamoja na kuajiri vijana wenzao,
kupanua mitaji ya biashara zao, kulipa karo za shule za watoto wao na
kujikwamua kimaisha tofauti na ilvyokuwa awali kaba hawajapata mkopo na kufanya
shughuli za ujasiriamali.
Kwa upande wake mkazi wa kijiji cha Ibwera Ibrahim Mulokozi
ambaye alipata mkopo wa shilingi laki nne kupitia SACCOS ya kijiji hicho
alisema kuwa ameweza kununua matandazo na kulipa wasaidizi wanaohudumia shamba lake la migimba na kahawa ambalo
ni la mfano kwa vijana na wazee wanaotoka kata ya Ibwera, Mikoni na Nyakibimbili
na kwenda kujifunza na kuchukua miche ya
migomba.
Alisema kuwa anakabiliwa na changamoto za kutokuwa na fedha
za kuendeleza shughuli za kilimo, kutoka na mbolea ya kutosha ya kurutubisha
shamba, bei ya miche ya kahawa kupanda kutoka shilingi 50 hadi 500 kwa mche
mmoja, kuendelea kutumia jembe la mkono, kutokuwa na masoko ya uhakika hasa
soko la ndizi na magonjwa ya migomba.
Naye katibu wa
kikundi cha Msifuni Johanes Joel
ambacho kilipata mkopo wa shilingi milioni moja na laki tano kutoka Halmashauri ya wilaya ya Bukoba alisema kuwa kikundi chao kinajishughulisha
na kazi ya ukulima wa samaki na walianza na bwawa moja na hivi sasa wana
mabwawa matatu na wanampango wa kuhakikisha kuwa kila mwanakikundi anakuwa na bwawa lake.
“Changamoto zinazotukabili ni kutokuwa na mtaji wa kutosha,
wanachama kutokuwa na elimu ya kuendesha na kusimamia au kutunza miradi na
kufanyiwa hujuma kwa mradi wetu wa samaki
ikiwa ni pamoja na kuibiwa na
kuharibiwa kwa mabwawa hasa nyakati za usiku na watu wasiopenda kufanya kazi za
maendeleo”, allisema Joel.
Kwa upande wake waziri Dk. Mukangara aliwataka vijana wa
kijiji hicho kufanya kazi kwa kujituma na kujiunga katika vikundi vya maendeleo
jambo ambalo litawafanya waweze kupata mikopo kutoka mfuko wa maendeleo ya
vijana na halmashauri ya wilaya na hivyo kuweza kujishughulisha na kazi za upandaji wa miti, kilimo cha samaki na
ufugaji wa ng’ombe wa maziwa na nyuki.
Dk. Mukangara alisema, “Vijana ni lazima mfanye kazi na kuachana na tabia ya
uvivu, kufanya kazi si lazima uajiriwe
bali unaweza kujiajiri wewe mwenyewe kama hapa Ibwera kunahali ya hewa nzuri na
milima mingi haina miti mnaweza kuwa na mradi wa kupanda miti na kufuga nyuki
ambao watawapatia asali na mkiiuza mtapata fedha nahivyo kujikwamua kiuchumi”.
Kwa upande wa mafunzo ya ujasiriamali waziri Dk. Mukangara
alisema kuwa wizara yake inavituo vya kuwajenge uwezo vijana hivyo basi kama
wahusika ambao ni vijana watakuwa tayari
kupata mafunzo ya ushirika na mafunzo mengine kama ya uongozi, stadi za maisha
watayapata na yatawasaidia katika maisha
yao.
Waziri Dk. Mukangara alikuwa mkoani Kagera kwa ajili ya
kukagua SACCOS na vikundi vya vijana
vilivyopata mkopo kutoka mfuko wa maendeleo ya vijana ili kuona fedha
hizo zimewasaidiaje vijana kujikwamua
kiuchumi. Katika wilaya ya Bukoba alilitembelea shamba la mfano la kahawa na
migomba, kikundi cha burudani cha Rugazi
na shamba la samaki la kikundi cha
Msifuni.
EmoticonEmoticon