Maelfu ya watu wamejiunga katika
maandamano ya amani katika mji mkuu wa India, Delhi, kupinga kitendo
kilichosababisha kifo cha mwanamke mmoja ambaye alibakwa na kundi la wanaume
mjini humo.
Mwanamke huyo mwenye umri wa
miaka 23, ambaye bado hajatambuliwa, amekufa kutokana na na majeraha Jumamosi
huko Singapore alikopelekwa kupata matibabu maalum.
Wanaume sita wanaoshikiliwa
kuhusiana na tukio la kumbaka mwanamke huyo, sasa wamefunguliwa mashitaka ya
mauaji.
Shambulio hilo la aibu
lilifanyika tarehe 16 Desemba 2012 na kusababisha maandamano kupinga
unyanyasaji wanaofanyiwa wanawake nchini India.
Maafisa wawili wa polisi tayari
wamesimamishwa kazi.
Mwili wa mwanamke huyo
unarejeshwa India katika mazishi yatakayofanyika kwa siri kuepusha ghasia zaidi
za waandamanaji.
"Kwa kweli wanawake wengi
nchini India wanakabiliwa na kitisho katika maisha yao katika mambo mbalimbali
kama vile kunapozuka ghasia, ukosefu wa huduma za afya, kukosekana kwa usawa,
kupuuzwa, lishe duni, kutojaliwa kwa afya ya mtu na utu wake"
Polisi wa kuzuia ghasia wamefunga
eneo la katikati ya Delhi ili kuzuia maandamano zaidi.
Waziri mkuu wa India Manmohan
Singh amesema anaelewa hasira ya wananchi, ametaka hatua zaidi zichukuliwe ili
kufanya India kuwa mahali salama kwa wanawake kuishi.
Maandamano pia yamefanyika katika
miji mingine ya India ikiwemo Calcutta, Bangalore na Mumbai.
Mwandishi wa BBC, India anasema
kwa zaidi ya wiki mbili, mwanamke huyo ambayo hajatambulishwa amekuwa ishara ya
mateso makubwa wanayopata wanawake wengi nchini humo.
Amesema, hata baada ya mazishi,
mawazo yataendelea, kwa wananchi kuisukuma serikali kuchukua hatua kuhakikisha
namna haki za wanawake zinavyoweza kulindwa.
CHANZO: BBC NEWS
EmoticonEmoticon