Serikali za Tanzania na Malawi zimefikia makubaliano ya
kumtafuta mpatanishi wa kimataifa atakayetatua hitilafu za mpaka wa majini kati
ya nchi hizo mbili.
Bernard Membe Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Tanzania
ameyasema hayo mjini Dar es Salaam alipokutana na mwenzake Ephrahim Muganda
Chiume wa Malawi na kuongeza kuwa, pande hizo mbili zimechukua uamuzi wa pamoja
wa kuupeleka mgogoro huo kwa jopo la maraisi wastaafu wa Afrika linaloongozwa
na Joaquim Chissano Rais wa zamani wa Msumbiji ambalo linashughulikia kutatua
hitilafu na migogoro mbalimbali barani
Afrika.
Pande hizo mbili zimeafikiana kwamba, iwapo hazitaridhishwa na
maamuzi ya upatanishi huo, zitalazimika kuwasilisha hitilafu zao kwenye Mahakama
ya Kimataifa ya Haki ICJ. Malawi inadai kwamba mpaka wa nchi hizo mbili upo
kwenye ufukwe wa Tanzania kwa maana kwamba nchi hiyo haina haki ya kutumia maji
ya ziwa hilo ambalo linahesabiwa kuwa ni la tatu kwa ukubwa barani Afrika.
Hii
ni katika hali ambayo, Tanzania nayo inadai kuwa mpaka wa nchi hizo mbili uko
katikati ya maji ya ziwa Nyasa. Mgogoro kati ya Tanzania na Malawi ulianza
mwezi Julai mwaka huu baada ya Malawi kuanza kufanya utafiti wa mafuta katika
eneo la Tanzania, hali ambayo ilisababisha serikali hizo mbili kuanza
kulumbana. Inasemekana kuwa, chini ya maji ya ziwa hilo kuna utajiri mkubwa wa
mafuta na gesi.
EmoticonEmoticon