KESI ya msanii wa fani ya filamu nchini, Elizabeth Michael
maarufu kama Lulu, imeendelea kupigwa kalenda kutokana na upelelezi wake
kutokukamilika.Lulu anakabiliwa na kesi ya mauaji ya msanii mwenzake, Steven
Kanumba, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akidaiwa kutenda kosa hilo
nyumbani kwa marehemu Aprili 7, mwaka huu.
Kesi hiyo inayosikilizwa na Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo,
Agustina Mmbando, jana ilitajwa mahakamani hapo lakini kwa mara nyingine upande
wa mashtaka uliendelea kudai kuwa upelelezi haujakamilika.Wakati kesi hiyo
ilipotajwa Novemba 5, mwaka huu kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilisha
ili hatua nyingine ziweze kufuata, Wakili wa Serikali, Seth Sekwao alidai
upelelezi haujakamilika.
Kutokana na taarifa hiyo ya upande wa mashtaka, mmoja wa
mawakili wanaomtetea mshtakiwa, Peter Kibatala alitaka kuharakisha upelelezi wa
kesi hiyo, ili iweze kusonga mbele.
Wakili Kibatala, ambaye pia ni Makamu Rais wa Chama cha
Wanasheria Tanganyika (TLS), alidai kila mara upande wa mashtaka umekuwa ukidai
upelelezi haujakamilika, jambo ambalo linaifanya kesi hiyo ishindwe kuendelea
katika hatua nyingine.
“Ni muda mrefu sasa, kesi hii imekuwa ikitajwa mara kwa mara
upande wa mashtaka umekuwa ukidai upelelezi haujakamilika. Hivyo tunawakumbusha
upande wa mashtaka ujitahidi kuharakisha upelelezi ili iweze kusonga mbele,”
alidai Wakili Kibatala.
Upande wa mashtaka uliiomba mahakama ipange tarehe nyingine
ya kutajwa.
Hakimu Mmbando aliahirisha kesi hiyo hadi Desemba 3, mwaka
huu itakapotajwa tena kwa ajili ya kuangalia kama upelelezi utakuwa
umekamilika.Lulu alipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Aprili 11, mwaka huu
na kusomewa shtaka moja la mauaji ya msanii mwenzake, Kanumba.
Akimsomea shtaka hilo, Wakili wa Serikali Mwandamizi,
Elizabeth Kaganda alidai Aprili 7, mwaka
huu eneo la Sinza Vatcan alimuua msanii, Steven Kanumba.
EmoticonEmoticon