Katibu Kuu Wa CHADEMA, Dr. Willibroad Slaa
ADAI WATEULE WAPYA WANA TASWIRA YA UFISADI
KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),
Dk. Willibrod Slaa, ameichambua safu mpya ya uongozi wa Chama cha Mapinduzi
(CCM) iliyoundwa hivi karibuni mjini Dodoma, akisema wana taswira ya ufisadi.
Amesema kuwa hali hiyo inatokana na baadhi yao kuhusika
kwenye matukio kadhaa ya kifisadi moja kwa moja.
Akizungumza na Tanzania Daima jana kuhusu mtazamo wake kwa
safu hiyo mpya ya uongozi wa CCM iliyoundwa na Mwenyekiti wake, Rais Jakaya
Kikwete, katika mkutano mkuu uliomalizika juzi, Dk. Slaa alisema haoni jambo
jipya.
“Nadhani hakuna jambo jipya, kipya ni kwamba wameteuliwa
jana, lakini wote ni wazoefu wachafu,” alisema.
Katika safu hiyo, Kikwete anasaidiwa na makamu wawili,
Philip Mangula wa bara na Dk. Ali Mohamed Shein wa visiwani na pia alimteua
kada mkongwe, Abdullahman Kinana kuwa Katibu Mkuu mpya wa CCM.
Wengine wanaounda Sekretarieti ni Zakhia Meghji, Mwigulu
Nchemba, Asha-rose Migiro, Vuai Ali Vuai, Nape Nnauye na Mohamed Seif Khatib.
Akimchambua mmoja baada ya mwingine, Dk. Slaa alimtuhumu
Mangula kuwa ni mmoja wa watu waliohusika na ufisadi wa fedha za Akaunti ya
Malipo ya Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania.
“Makamu Mwenyekiti Mangula anahusika na EPA, vimemo vingi
vya kutaka fedha za EPA vimetokea kwake…sioni leo atajisafishaje kuleta tumaini
jipya kwa Watanzania,” alisema.
Kuhusu Meghji, Dk. Slaa alisema huyo ndiye aliyeandika barua
na kudanganya kuwa fedha hizo za EPA zimetoka kwa ajili ya Usalama wa Taifa.
“Sasa mtu kama huyo aliyedanganya, leo hii ukamweka kwenye
fedha maana yake ni ku-‘recycle material’ ile ile,” alisema Dk. Slaa.
Akimchambua Katibu Mkuu, Kinana, alisema kigogo huyo ana
mkono katika biashara chafu za makampuni ya meli na kwamba hajakanusha mpaka
sasa.
Dk. Slaa alisema Kinana ambaye alikuwa meneja kampeni wa
mgombea urais wa CCM mwaka 2010, katika chaguzi hizo CCM imeshutumiwa kwa kuiba
kura, hivyo uteuzi wake ni kukubali kuzika demokrasia nchini.
Alisema timu hiyo imeundwa mahsusi kwa ajili ya kujiandaa
kuiba kura mwaka 2015.
Dk. Slaa aliongeza kuwa baada ya uchaguzi, CCM walitumia
fedha nyingi kwa ajili ya kwenda kufanya utafiti wa kukijenga upya chama chao,
ambao uliozaa kauli mbiu ya ‘Kujivua Gamba’, kwamba pamoja na kazi ya kitaalamu
wameshindwa kuvuana magamba.
Alifafanua kuwa hatua hiyo inatokana na ukweli kwamba
walioitwa magamba sasa wamo kwenye safu mpya ya uongozi wa CCM.
Katika kile kinachoonekana kuwa ni kumjibu Rais Kikwete hasa
kutokana na kauli yake kuwa wapinzani wanafanya kazi ya kueneza uongo na
kuwataka makada wa CCM kujibu mapigo, Dk. Slaa alimtaka aache kuwadanganya
Watanzania.
Dk. Slaa alisema kuwa Rais Kikwete huenda hasomi,
anadanganywa au anapenda lugha rahisi za kusema wenzake waongo.
“Mawaziri wameutumia Mkutano Mkuu kwa mbwembwe kueleza
uongo…katika ripoti ya Juni 2012, hali ya uchumi wa taifa, iliyoandikwa na
Ofisi ya Rais, Ofisi ya Mipango, na kelele zote zilizopigwa kuhusu maendeleo
yaliyopatikana kwenye barabara.
“Kwenye ripoti hiyo imeandikwa kuwa mwaka 2011 barabara
zilizokuwa katika hali nzuri ni kilomita 5,976 sawa na asilimia 30.4 ya
barabara zote za mikoa,” alisema.
Ukilinganisha na mwaka 2010, barabara zilizokuwa na hali
nzuri ni kilomita 11,012, maana yake ni kuwa nusu ya barabara zilizokuwa nzuri
mwaka 2010 leo mwaka mmoja baadaye ni mbaya.
Aliongeza kuwa wakizitumia takwimu hizo ambazo zimeandikwa
na Ofisi ya Rais, bado wanaambiwa ni waongo.
Alisema itakumbukwa kwenye viwanja vya Mwembe Yanga wakati
alipotoa orodha ya mafisadi, Rais Kikwete alimjibu kuwa kelele za mlango
hazimzuii mwenye nyumba kulala lakini leo amekiri ufisadi upo CCM.
Mwanasiasa huyo machachari, alisema kuwa Rais Kikwete
amesikika mara kadhaa akilalamika kuhusu ufisadi ndani ya chama chake na kuhoji
kati yake yeye na Kikwete nani muongo?
“Aidha Rais sio makini; anapenda maneno rahisi…tunamwambia
aweke hadharani takwimu asilete propaganda,” alisema.
Slaa alikumbusha pia jinsi ambavyo Rais Kikwete na CCM
walivyowaita ni waongo wakati CHADEMA walipokuja na sera ya matumaini kwa
Watanzania mwaka 2010, wakisema nyumba za tembe na nyasi sasa basi na kueleza
mikakati yao ya kushusha bei ya saruji na vifaa vya ujenzi.
Katika hilo Dk. Slaa alisema kuwa alifurahi juzi kusikia CCM
katika maazimio ya Mkutano Mkuu wao wakisema kuwa watashusha bei ya saruji na
vifaa vya ujenzi.
“Sasa CCM na CHADEMA nani waongo? Mimi nasema hakuna kitu
kinachotushangaza katika uongozi wa sasa, timu ni ile ile ya mafisadi,” alisema
Aliwataka Watanzania kuwa makini akidai kuwa waliowekwa
kwenye safu ya uongozi CCM ni mafundi wa ufisadi na kutoa wito kuwa wajiandae
kulinda kura.
Naye Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi Samuel Ruhuza, alisema wao
kama chama wanawapongeza CCM lakini kwa jicho la siasa hawaoni kipya na kwamba
viongozi wapya ni wachovu wale wale.
“Hawana jambo jipya kwa sababu CCM imechoka sana haina watu
wapya ni walewale, sasa hivi tulitegemea vijana wapya lakini hilo halijatokea,”
alisema Ruhuza.
JK awasuta wabaya CCM
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Taifa (CCM), Rais Jakaya
Kikwete, amewashambulia wanachama wa chama hicho waliokuwa na ndoto za kuona
mkutano mkuu wao ukimalizika kwa mpasuko, akisema kuwa wameshindwa.
Rais Kikwete alitoa kauli hiyo jana ikiwa ni siku moja baada
ya kuiteua sekretarieti ya chama hicho, itakayoongozwa na Katibu Mkuu,
Abdullahman Kinana.
Akiwatambulisha rasmi wateule hao, Rais Kikwete alisema
anawashangaa baadhi ya wanachama ambao wanaifahamu vizuri CCM lakini walikuwa
wakiombea mabaya ili mkutano umalizike vibaya waweze kujivunia kile
walichokikusudia.
“Namshukuru sana Mungu tumemaliza salama; kuna watu walikuwa
wakitambika usiku na mchana CCM imalize vibaya mkutano wake na walitamani itoke
na vipande lakini wameshindwa na sijui watamdai nani gharama zao?” alihoji.
Alisema watu hao wamepoteza muda wao bure na CCM imara
imeweza kumaliza mkutano wake vizuri na kupanga safu ya ushindi katika uchaguzi
wa serikali za mitaa pamoja na kuingia Ikulu mwaka 2015.
“Nimesikia mambo mengi na kuna watu kabisa walikuwa
wakinijia wakiniambia kuwa kuna jambo hili na hilo, lakini nilikuwa nawaambia
kuwa watulie kwani kuna watu wana ndoto za mchana wanatumia nguvu nyingi,
wanatumia muda wao bure na wanapoteza wakati wao,” alisema.
Rais Kikwete alitamba kuyatekeleza maazimio yote
waliyoazimia moja baada ya lingine ili kuhakikisha wanayatimiza kwa wakati na
kwa muda mfupi ili Watanzania kuendelea kujenga imani na chama hicho.
Alisema wajumbe wa NEC wanatakiwa kutumia muda wao mwingi
kuifanya kazi ya chama ili kuweza kukijenga chama hicho kwa kiwango kikubwa.
EmoticonEmoticon