Kamanda wa Polisi Mkoani Mbeya, DIWANI ATHUMAN
MBEYA, Tanzania
JESHI la Polisi mkoani Mbeya linawashikilia watu 10 wanaodhaniwa kuwa ni askari wa Jeshi
la Wananchi Tanzania (JWTZ) kikosi cha 44 KJ
Kambi ya mji mdogo wa Mbalizi kwa
tuhuma za mauaji ya mkazi wa mji huo, Petro Sanga (25).
Askari hao wanadaiwa kumuua Sanga kwa kumchoma kisu shingoni
na mdomoni, kisha kuwajeruhi watu wengine sita kwenye Baa iitwayo Power Night,
ambako walikwenda kwa lengo la kulipiza kisasi cha kupigwa kwa askari mwenzao,
Geodfery Matete (30).
Hata hivyo, Matete anadaiwa kwamba alikuwa amepigwa na
walinzi wa kilabu cha pombe cha DDC kilichopo katika mji huo wa Mbalizi,
Novemba 18 mwaka huu saa 3 usiku.
Mauaji hayo yamekuja siku moja baada ya Mahakama Kuu Kanda
ya Dar es Salaam kuwahukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa
askari watatu wa JWTZ na JKT, baada ya
kupatikana na hatia ya kumuua, Swetu
Fundikira.
Hata hivyo, askari hao waliohukumiwa kunyongwa, jana
waliwasilisha taarifa ya kusudio la kukata rufaa katika Mahakama Kuu ya Tanzania.
Kamanda wa Polisi mkoani wa Mbeya, Diwani Athuman
alithibitisha mauaji hayo mapya yaliyotokea katika Mji wa Mbalizi na kwamba
marehemu Sanga alikutwa na mauti akiwa anakunywa pombe kwenye baa iitwayo Power
Night.
“Marehemu na wenzake walivamiwa na askari hao na kuanza
kuwashambulia. Askari hao waliwashambulia wananchi waliokuwapo kwenye baa hiyo
na Sanga alifariki dunia baada kupigwa sehemu mbalimbali za mwili wake kwa
mateke, mikanda, marungu, sime na mapanga,” alisema Kamanda Athuman na
kuongeza:
“Baada ya kumpiga walimchoma
kisu mdomoni. Katika jitihada zake za kujiokoa, marehemu alikimbilia
katika baa nyingine ya Vavenemwe.”
Kwa mujibu wa Kamanda Athuman, baada ya marehemu kufika
katika baa hiyo alipoteza fahamu na wasamaria wema walimbeba na kumkimbiza
katika Hospitali Teule ya Ifisi iliyopo katika mji huo mdogo.
“Alifariki wakati akipatiwa matibabu na hiyo ilitokana na
kuvuja damu nyingi,” alisema.
Chanzo cha vurugu
Kamanda Athuman alisema chanzo cha vurugu hizo, ni askari wa JWTZ, Matete
(30) kushambuliwa na walinzi wa kilabu
cha pombe za kienyeji kilichojulikana
kwa jina la DDC Novemba 17 mwaka huu.
Alisema kuwa kutokana
na tukio hilo, Polisi wanawashikilia
walinzi wanne kwa mahojiano zaidi ambao ni Frank Mtasimwa (25), Mure
Julius (26), Omari Charles (28) na Regnad Mwampete, wote wakazi wa Kijiji cha
Izumbwe Wilaya ya Mbeya.
Kamanda Athuman alisema majina ya askari waliokamatwa kwa
tuhuma hizo yatatajwa baadaye kwani bado uchunguzi unaendelea huku akivitaka
vyombo vya dola kuacha kujichukulia sheria mkononi kwa kuwa hali hiyo inaweza
kusababisha uvunjifu wa amani.
“Uchunguzi wa tukio hili ukikamilika waliokamatwa
watafikishwa mahakamani” alisema.
Msemaji wa JWTZ, Kanali Kapambala Mgawe alisema kuwa hana
taarifa za wanajeshi hao kufanya mauaji huku akisisitiza kuwa kama
wanashikiliwa na Jeshi la Polisi ni wazi kuwa watakuwa wanahusika na tukio
hilo.
“Bado sijapata taarifa rasmi kuhusu tukio hilo kwa kuwa hivi
sasa sipo katika eneo la kazi, polisi ndio wanaweza kusema lolote na kama kweli
wanawashikilia basi watakuwa wamehusika,” alisema Mgawe.
Walioua na rufaa
Wakati huohuo, askari
watatu wa JWTZ, waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya
kupatikana na hatia ya kumuua Swetu
Fundikira, jana wamewasilisha taarifa ya kusudio la kukata rufaa katika Mahakama Kuu ya Tanzania.
Wakili wa askari hao, Mluge Karoli alisema wamewasilisha
kusudio hilo la taarifa ya kukata rufaa kwa sababu hawajaridhishwa na uamuzi
uliotolewa na Jaji Zainabu Muruke wa
kuwatia hatiani wanajeshi hao kwa kosa la kumuua kwa makusudi Fundikira,
kinyume cha kifungu cha 196 cha Kanuni za Adhabu.
Karoli akitoa sababu za kuwasilisha kusudio hilo la kukata
rufaa alidai kuwa kesi yoyote ya ugomvi
haiwezi kuwa na kusudio la kutaka
kuua na kwamba hakuna shahidi aliyefika mahakamani hapo na kueleza kuwa wateja
wake ndio wamemuua Swetu Fundikira.
Pia alienda mbali zaidi na kudai kuwa wateja wake ambao ni
MT 1900 Sajini Roda Robert (42), MT 85067 Koplo Mohamed Rashid wa JKT Mbweni na MT 75854 Koplo Ally Ngumbe
(37) wa kikosi cha JWTZ Kunduchi hawakuwa na wajibu wa kuthibitisha mauaji
hayo.
“Waliomuua marehemu Swetu siyo wateja wangu na
ninaamini Mahakama ya Rufani itaangalia
upya ushahidi na kutenda haki,” alidai Karoli.
Aliongeza kudai kuwa aliyepambana na wateja wake ni Swetu
Fundikira na uchunguzi wa daktari unaonyesha jina la Swetu Ramadhani Fundikira
hivyo ni watu wawili tofauti na kwamba hakuna hata shahidi mmoja aliyesema aliwahi kuona mwili wa marehemu ama
kuhudhuria kwenye msiba.
Askari hao kwa pamoja wanadaiwa kuwa walimpiga Fundikira,
Januari 23 mwaka huu saa 7:30 usiku
wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam na baadaye kufariki dunia usiku huohuo
wa kuamkia Januari 24, mwaka 2010, katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Hukumu hiyo iliyotolewa juzi na Jaji Mruke, ilifufua upya
msiba wa Swetu, baada ya ndugu zake kuangua vilio, huku chumba cha Mahakama
kikigeuka kwa muda kuwa sehemu ya msiba.
Sambamba na vilio hivyo, ndugu wawili wa marehemu Swetu
walianguka chini na kuzirai kwa muda, kabla ya kupewa huduma ya kwanza na
kurejea katika hali ya kawaida.
Akisoma hukumu hiyo, Jaji Muruke alisema ingawa hakuna
ushahidi wa moja kwa moja kuwa washtakiwa hao ndio waliomuua Fundikira,
ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka
(Jamhuri) ulikuwa ni ushahidi wa mazingira, kwamba Jamhuri imeweza kuthibitisha
mashtaka hayo.
Alisema kuwa anakubaliana na mtiririko wa ushahidi wa upande
wa mashtaka kama ulivyoelezwa na mashahidi wake sita akiwamo daktari
aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu, askari polisi wawili ambao washtakiwa
katika utetezi wao walishindwa kuuvunja.
“Sheria iko wazi ukiondoka na mtu au ukionekana naye kwa
mara ya mwisho na baadaye mtu huyo akapatikana na madhara, wewe ndio
unawajibika kutoa maelezo ya kina kuhusu yaliyompata mtu huyo” alisema Jaji
Muruke na kuongeza;
“Kisheria ukitoa maelezo ambayo hayajakidhi haja na yana
utata ni faida kwa upande wa mashtaka ambao hutegemea ushahidi wa mazingira.
Maelezo ya kina hayajatolewa na washtakiwa wote.”
Aliendelea, “Ushahidi
wa Jamhuri japokuwa ni wa mazingira, umejengwa thabiti na upande wa utetezi
haukuweza kujenga matundu, ama kuuvunja mnyororo huo, kidole kinawaelekea wao.”
Jaji Muruke alisisitiza kuwa katika kesi hiyo licha ya kuwa
kuna ushahidi wa kimazingira, upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha mashtaka
bila kuacha shaka.
“Hivyo kosa wanaloshtakiwa nalo limethibitishwa na Mahakama
imewaona washtakiwa kuwa wana hatia ya kumuua Swetu Abdallah Fundikira” alisema
Jaji Muruke.
EmoticonEmoticon