Na Fredy Azzah na Kelvin Matandiko
MATOKEO mabaya ya mtihani wa kidato cha nne yamezidi kuibua
mapya, baada ya wamiliki wa shule na vyuo binafsi nchini kusema mitihani
ilitungwa kwa mfumo tofauti na uliozoeleka miaka yote, huku tume iliyounndwa na
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ikipondwa na baadhi ya watu.Mwenyekiti wa Chama cha
Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi nchini (TAMONGSCO), Mahmoud Mringo alisema
kwamba maswali waliyoulizwa watahiniwa yalikuwa ya kujieleza tofauti na miaka
ya nyuma, ambapo
mfumo uliotumika uliwataka watahiniwa kutaja vitu tu bila ya
kulazimika kuvielezea kwa undani.
Kauli yake iliungwa mkono na Mkuu wa Taaluma katika Shule ya
Sekondari ya Wasichana ya Marian, Florence Mapunda ambaye alisema kuwa mtihani
wa mwaka jana ulitaka zaidi watoto kujieleza tofauti na
miaka ya nyuma wakati
wanafunzi walipokuwa wanakariri.
Hata hivyo, Msemaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta),
John Nchimbi alisema mfumo wa mtihani haukubadilika kwa namna yoyote na kuwa
upo kama ule wa miaka yote.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philip Mulugo,
kwa upande wake alisema madai yanayotolewa hayana msingi, huku akihoji kwa nini
yasitoke tangu mitihani ilipokuwa ikifanyika na badala yake yanatoka baada ya
kutangazwa kwa matokeo.
Matokeo ya mtihani wa kidato cha nne uliofanyika mwaka jana
yanaonyesha kuwa watahiniwa 240,903 sawa na asilimia 60.6 wamepata sifuri, huku
wanafunzi 23,520 tu ambao ni sawa na asilimia 5.16 ndiyo waliofaulu na wengine
103,327 sawa na asilimia 26.02 wamepata daraja la nne.
Kutokana na matokeo hayo, Waziri Mkuu Pinda, juzi alitangaza
kuunda tume ya kuchunguza chanzo cha matokeo hayo kuwa mabaya, hatua ambayo
hata hivyo imekosolewa na wasomi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Tume hiyo inayoundwa na wajumbe kutoka Taasisi za Elimu,
Chama cha Waalimu, Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii na Umoja wa Wakuu wa
Shule za Sekondari Tanzania (Tahossa) inatarajiwa kuanza kazi wiki hii.
Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
alisema kuunda tume ni kupoteza muda kwa sababu matatizo na changamoto zote
ndani ya sekta hiyo yanajulikana, huku mwenzake, Profesa Chriss Maina pia wa
UDSM akisema kuunda tume hakutaisaidia kwa kuwa Serikali inaidharau sekta ya
elimu.
“Tatizo ni kutowekeza kikamilifu katika sekta ya elimu,
imekuwa na matumizi makubwa katika mambo yasiyokuwa ya lazima,”alisema Profesa
Mpangala.
Alisema matatizo mengine ni mazingira magumu ya kufundisha
na uhaba wa walimu. “Kinachotakiwa wajipange kufanyia kazi changamoto hizi
zilizopo badala ya kuunda tume, wakati fedha nyingi tunasikia inapotea kwenye
ubadhirifu,”alisema Profesa Mpangala.
Naye Profesa Maina alisema: “Hiyo tume ya kazi gani kwa
sababu matatizo yanafahamika wazi, umewahi kusikia taifa gani ambalo halina
mtalaa wa elimu. Hiyo ndiyo hali halisi kwa nchi yetu. ”
EmoticonEmoticon