Inaripotiwa kuwa Spika wa Bunge, Anne Makinda, amepokea
jumbe za maneno 400 na za miito ya simu 200 zenye matusi ya nguoni kutoka kwa
watu wakimtaka ajiuzulu.
Aidha inasemekana kuwa amesemea jumbe hizo zimerekodiwa.Kwamba, Spika alianza kupokea jumbe
hizo kuanzia juzi, baada ya viongozi wa CHADEMA kutangaza namba za simu za
Spika kwenye mkutano wa hadhara na kuendelea jana ili kutumia ‘nguvu ya umma’,
kumlazimisha ajiuzulu.
Sababu ya kutumwa jumbe hizo inaripotiwa kuwa ni baada ya
hatua ya Spika Makinda kutangaza mabadiliko ya Kamati za Bunge, yaliyoivunja
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) na shughuli zake kuwekwa
chini ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) ambapo katika mabadiliko hayo,
aliyekuwa Mwenyekiti wa POAC, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe
hakuridhishwa nayo na hivyo kumshitaki Spika Makinda kwa Wananchi ili wamng’oe.
Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashilillah alisema uamuzi huo
haukufanywa na Spika Makinda peke yake, bali ni baada ya kushauriana na Kamati
ya Kanuni za Bunge, ambayo iliridhika na sababu za kuchukuliwa uamuzi huo.
Wajumbe wa Kamati iliyoridhia makubaliano hayo mbali na
Spika na Naibu Spika, ni Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Mbunge wa
Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA). Wengine ni Mbunge wa Mbulu, Mustapha
Akunaay (CHADEMA), Mbunge wa Kibondo, Felix Mkosamali (NCCR-Mageuzi), Mbunge wa
Mkanyageni, Mohamed Habib Mnyaa (CUF) na Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed
(CUF). Pia Mbunge wa Viti Maalumu, Anna Abdallah (CCM), Mbunge wa Bariadi
Magharibi, Andrew Chenge (CCM), Mbunge wa Tunduru Kaskazini, Ramo Makani (CCM),
Mbunge wa Viti Maalumu, Pindi Chana (CCM) na Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod
Mkono (CCM).
CHANZO : HABARI LEO
EmoticonEmoticon