RAIS wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein, amepokea kwa mshtuko
mauaji ya Padri Evaristus Mushi na kutoa pole kwa waumini, ndugu jamaa, marafiki na wananchi
wote wa Zanzibar kufuatia kifo hicho.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais Mhe. Mohamed
Aboud ameeleza hayo jana, Jumatatu, Februari 18, 2013 na kusisitiza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa
kushirikiana na Jeshi la Polisi itawasaka hadi kuwatia mikononi na hatimaye
kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria wale wote waliohusika na mauaji hayo.
Waziri Aboud ameyaeleza hayo wakati alipozungumza na
waandishi wa habari ofisini kwake Vuga, kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein kufuatia mauaji
ya Padri Evaristus Mushi wa Kanisa
Katoliki Zanzibar Parokia ya Mtakatifu
ST.Joseph, Shangani.
Hapo jana Dkt. Shein alikutana na Askofu Augustino Shao wa
Kanisa Katoliki, Jimbo la Zanzibar, huko katika Ikulu Ndogo Migombani,
Zanzibar na kueleza masikitiko yake
kutokana na mauaji hayo ya Padri Mushi wa Kanisa Katoliki la Zanzibar, na
kuelezea haja ya kuwepo kwa uvumilivu katika kipindi hichi cha msiba.
Katika mazungumzo na waandishi wa habari, Waziri Aboud alisema kuwa Serikali imejipanga
vizuri kupitia vyombo vyake vya ulinzi
na usalama ili kuhakikisha kuwa watu wote waliohusika na mauaji hayo
wanakamatwa mara moja .
“Kutokana na jiografia ya Zanzibar,Tunaelewa kwamba zipo
sehemu katika kisiwa cha Zanzibar ambazo wahalifu wanaweza kuzitumia, hivyo
Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo husika vitaziba mianya yote ili
kupambana na uhalifu “, alisema Aboud.
Alisema matendo ya uhalifu yanafanywa katika mazingira ya
usiri mkubwa kwa hivyo ili wahalifu hao wakamatwe wananchi hawana budi kutoa
mashirikiano kwa Jeshi la Polisi pale
wanapohitajika.
Akijibu suali la Mwandishi, Mhe.Aboud alikanusha taarifa
zilizozagaa mitaani za kuwepo silaha nyingi mikononi mwa watu wasiohusika na
kuwataka wananchi kuondoa hofu.
Sambamba na hayo, Mhe. Aboud amewataka viongozi wa dini
mbali mbali pamoja na waumini wa dini
zote hapa Zanzibar kuwa wastamilivu
katika kipindi hiki kigumu cha maombolezi.
Aidha, Waziri Aboud alisisitiza haja ya kuwepo uvumilivu kwa
waumini wa dini zote ili kuirejesha Zanzibar katika historia yake ya kutokuwa
na migongano ya kidini.
EmoticonEmoticon