REPIN ROCK CITY

REPIN ROCK CITY

TUMA TRACK YAKO

PIMENI KAULI ZENU NA VITENDO VYENU- JK AWAAMBIA VIONGOZI WA DINI NA SIASA

11:07:00 PM

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewataka viongozi wa dini na wanasiasa kupima kauli na vitendo vyao ili kuepusha kuligawa taifa kwa misingi ya imani za dini na itikadi za siasa, kama ilivyotaka kujitokeza mwaka 2012.

Katika salamu zake za Mwaka Mpya kwa Taifa juzi, Rais Kikwete alisema kwa mara ya kwanza mwaka  2012, Tanzania ilifikishwa kwenye hatari ya kutokea mgawanyiko wa Watanzania au hata mapigano kwa misingi ya dini zao.

“Nimeshalisemea jambo hili siku za nyuma na napenda kurudia leo kuwasihi Watanzania wenzangu kupima athari za kauli zetu na matendo yetu kwa mustakabali wa jamii yetu, nchi yetu na watu wake,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:

“Viongozi wa dini, waumini na viongozi wa siasa na wafuasi wao wanao wajibu maalumu wa kuhakikisha kuwa Watanzania wanaendelea kuishi kwa upendo, amani na ushirikiano bila kujali tofauti ya dini zao, makabila yao, rangi zao au maeneo watokako.”

Ingawa Rais Kikwete hakutaja mambo yaliyotaka kuligawa taifa mwaka jana, mwaka huo ulikumbwa na matukio kadhaa yaliyohusishwa na imani za kidini ikiwamo uchomaji wa makanisa katika Miji ya Zanzibar na Dar es Salaam.

Matukio mengine ambayo baadhi ya watu waliyahusisha na imani za dini ni vurugu zilizofanywa na wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa Kikundi cha Waislamu wa Taasisi za Jumuiya ya Kiislamu Tanzania ambazo ni pamoja na kuvamia Ofisi za Makao Makuu ya Wizara ya Mambo ya Ndani, Dar es Salaam na uvamizi wa maeneo ya wazi eneo la Temeke. Hata hivyo, watu kadhaa walikamatwa na kufunguliwa mashtaka katika mahakama mbalimbali nchini kwa tuhuma za ama kushiriki au kuongoza vurugu hizo.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »

MNADA BANNER