MAMLAKA ya Udhibiti
wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), imetangaza bei kikomo cha bidhaa za
mafuta kinayoonyesha kuwa petroli, dizeli na mafuta ya taa zimeshuka kuanzia
leo.
Taarifa iliyotolewa
jana na Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Haruna Masebu imesema bei hizo zimepungua
ikilinganishwa na toleo lililopita la Desemba 5, mwaka jana.
“Katika toleo hili,
bei za rejareja kwa petroli, dizeli na mafuta ya taa, zimepungua kwa viwango
vifuatavyo: petroli Sh126 kwa lita sawa na asilimia 5.96; dizeli Sh32 kwa lita
sawa na asilimia 1.60 na mafuta ya taa Sh50.74 kwa lita sawa na asilimia 2.50,”
imeeleza taarifa hiyo.
Kwa punguzo hilo, bei
ya rejareja ya petroli katika jiji la Dar es Salaam itauzwa kwa Sh1,993, dizeli
Sh1,967 na mafuta ya taa Sh1,973. Arusha petroli ni Sh2,077, dizeli Sh2,051 na
mafuta ya taa Sh2,057.
Katika jiji la Mbeya
petroli itauzwa kwa Sh2,099, dizeli Sh2,074 na mafuta ya taa Sh2,079 na jijini
Mwanza, petroli itauzwa kwa Sh2,142, dizeli Sh2,117 na mafuta ya taa Sh2,122.
Taarifa imefafanua
kuwa mbali na kupungua bei hiyo katika uuzaji wa rejareja, bei pia imepungua
kwa katika uuzaji wa jumla ikilinganishwa na matoleo mawili yaliyopita.
“Bei za jumla kwa
kulinganisha matoleo haya mawili zimepungua kama ifuatavyo: petroli kwa
Sh126.10 kwa lita sawa na asilimia 6.17; dizeli kwa Sh32.48 kwa lita sawa na
asilimia 1.69 na mafuta ya taa kwa Sh50.74 kwa lita sawa na asilimia 2.6,”
alisema.
Mkurugenzi huyo
amesema katika taarifa hiyo kuwa mabadiliko hayo ya bei, yametokana na kupungua
kwa bei ya mafuta katika soko la dunia na kuimarika kidogo kwa thamani ya
Shilingi ya Tanzania dhidi ya Dola ya Marekani.
Alisema kwa mujibu wa
Sheria ya Mafuta ya mwaka 2008, bei za bidhaa za mafuta ya petroli, zitaendelea
kupangwa na soko.
“Ewura itaendelea
kuhamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za bei kikomo za bidhaa za mafuta.
Taarifa hizi zina lengo la kuwasaidia wadau kufanya uamuzi stahiki kuhusu ununuzi
wa bidhaa za mafuta,” alisema Masebu.
Hata hivyo, Masebu
alisema pamoja na mpango huo wa Ewura kuweka bei ya kikomo, kampuni za mafuta
ziko huru kuuza bidhaa hizo kwa bei ya ushindani, ilimradi ziwe chini ya bei
hiyo kikomo.
Alivitaka vituo vya
mafuta kuchapisha bei hizo mpya katika mabango yanayoonekana bayana na
kuonyesha bei ya mafuta, punguzo, vivutio vya biashara au promosheni
zinazotolewa na kituo husika.
“Pale ambapo
inawezekana kuchagua, wateja wanashauriwa kununua bidhaa za mafuta kutoka kwenye
vituo vinavyouza mafuta kwa bei ndogo zaidi ili kushamirisha ushindani. Ni kosa
kuuza mafuta bila kuweka mabango ya bei inayoonekana vizuri kwa wateja na
adhabu itatolewa kwa kituo husika,” alisema.
Masebu aliwashauri
wanunuzi kuchukua stakabadhi ya malipo inayoonyesha jina la kituo, tarehe, aina
ya mafuta yaliyonunuliwa na bei kwa lita ili itumike baadaye kama kidhibiti
endapo kutajitokeza malalamiko ya ama kuuziwa mafuta kwa bei ya juu kuliko ya
kikomo au yenye kiwango cha ubora kisichofaa.
CHANZO : MWANANCHI
EmoticonEmoticon