Na: Daniel Mjema-Moshi
MTU aliyepiga picha na Mbunge wa Arusha mjini, Godbless Lema
akiwa amevalia sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), amehukumiwa
kifungo cha miaka minne jela. Abubakari Kikulu (29), alipiga picha na mbunge
huyo Desemba 23 mwaka jana, baada ya Lema kumaliza kuhutubia mkutano wa hadhara
eneo la Mererani, ikiwa ni sehemu ya mikutano aliyoifanya kutokana na Mahakama
ya Rufani Tanzania kumrejeshea ubunge wake.
Mbali na kupiga picha hiyo na Lema pamoja na Mbunge wa
Arumeru Mashariki Joshua Nassari, kijana huyo alionekana katika picha hiyo
akionyesha vidole viwili, ambayo ni alama ya Chadema.
Hata hivyo, baada ya picha hiyo, JWTZ lilimtilia shaka
kijana huyo na kutangaza rasmi kumsaka, ili lijiridhishe kama ni mmoja wa
wanajeshi wake.
Baada ya kumsaka kwa takriban siku 12, kijana huyo
alikamatwa Januari 13, katika Mji wa Bomang’ombe wilayani Hai na baada ya
kupekuliwa alikutwa na sare hizo.
Jana, Kikulu alifikishwa mahakamani mjini Moshi, akiwa chini
ya ulinzi wa polisi na kusomewa mashtaka mawili, ambayo yote alikiri kuyafanya
kama ilivyodaiwa mahakamani.
Baada ya kukiri kosa hilo Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama
ya Mkoa wa Kilimanjaro, alimhukumu kifungo cha miaka minne jela, ili iwe
fundisho wa wakosaji wengine wa aina hiyo.
Kabla ya hukumu hiyo, Wakili wa Serikali, Ignas Mwinuka
alimsomea mshtakiwa huyo mashitaka yake mawili, likiwamo la kujifanya Ofisa wa
Jeshi, wakati akijua ni uongo.
Wakili huyo alidai mahakamani kuwa Januari 3, mwaka huu
katika eneo la Bomang’ombe wilayani Hai, mtuhumiwa huyo alijitambulisha kama
mtumishi wa umma.
Katika shtaka la pili, wakili huyo alidai siku hiyo hiyo
katika Mtaa wa Msikitini, eneo hilo la Bomang’ombe, mtuhumiwa alipatikana na
sare za JWTZ kinyume cha sheria.
Sare hizo ni pamoja na suruali moja, mashati mawili na kofia
mbili, vyote vikiwa na alama za Jeshi la Wananchi wa Tanzania la Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Baada ya Hakimu Kobelo kumuuliza mshtakiwa kama ni kweli
alitenda makosa anayoshitakiwa, mshtakiwa huyo alikiri makosa yake katika hali
ambayo haikutarajiwa.
Kutokana na kukiri kwake makosa hayo, Hakimu Kobelo
alimhukumu kifungo cha miaka miwili kwa kosa la kwanza la kujifanya Ofisa wa
JWTZ na miaka mingine miwili kwa kosa la pili.
Hata hivyo, Hakimu Kobelo alisema kuwa kwa kuwa adhabu hizo
zinakwenda kwa pamoja (concurrent), mshtakiwa huyo atatumikia kifungo cha miaka
miwili jela.
Kwa mujibu wa hakimu huyo, kosa alilolifanya mtuhumiwa huyo
ni baya na linastahili adhabu kali, ili iwe fundisho kwa watu wengine
wanaotumia vibaya sare za majeshi nchini.
EmoticonEmoticon