Mkuu Wa Wilaya ya Makete, Mhe. Josephine Matiro akizungumza na wakazi wa Makete waliohudhuria Sherehe hizo hapo Jana
Na Edwin Moshi, Makete
Imeelezwa kuwa ni jambo la kushangaza na kusikitisha kuona
bado wanamakete wanakumbatia sababu zinazopelekea kuongeza kasi ya maambukizi
ya virusi vya UKIMWI licha ya elimu ya kujikinga na ugonjwa huo kuendelea
kutolewa siku hadi siku
Miongoni mwa sababu hizo zinazokumbatiwa na wanamakete ni
pamoja na kurithi wajane bila kupima wala kujua mumewe alikufa kwa UKIMWI ama
la, ulevi uliokithiri hasa wa pombe za kienyeji, kufanya ngono isiyo salama
pamoja na watu kutokubali kubadili tabia licha ya kupewa elimu ya namna ya
kujikinga na VVU
Hayo yamesemwa na mkuu wa wilaya ya Makete aliyekuwa mgeni
rasmi katika maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani Mh. Josephine Matiro, ambayo
kiwilaya imeadhimishwa katika kata ya Ikuwo tarafa ya Ikuwo wilayani hapa
Mkuu Wa Wilaya Makete Mhe.Josephine akiteta Jambo katika Meza Kuu
Amesema kwa hivi sasa kutokana na dhana iliyojengeka katika
maeneo mengine nje ya wilaya kuwa wilaya ya Makete inaongoza kwa kuwa na watu
wenye VVU, jambo ambalo amesema si kweli lakini pia dhana hiyo itaondoshwa
vichwani mwa watu huko nje ya wilaya kwa kuacha kukumbatia sababu zinazopelekea
ongezeko la VVU
“Unajua wakati nakuja Makete kila mtu alikuwa ananishangaa
wanasema Makete hakuna watu, wengi wamekufa kwa UKIMWI, lakini nashukuru
nimekuja na nimekuta watu, na si kweli kwamba wote mna VVU kama wanavyosema
lakini kikubwa tubadilike hivi sasa ili kuondoa hiyo hali zaidi ya hapa tulipo”
alisema Matiro
Mmoja wa Watumishi wa Shirika la SUMAMSESU Wilayani makete akiwa amevalia Tshirt Yenye Ujumbe Huu
Mkuu huyo ametoa agizo kwa viongozi wote wa kata na tarafa
ya Ikuwo kuhakikisha wanadhibiti wale wanaofungua vilabu ya pombe na baa muda
wa kazi kwani nao wanachangia ongezeko la VVU hiyo sheria ifuatwe kwa wale wote
watakaokaidi
Awali kabla ya kutoa hotuba yake kwa wananchi waliofurika
katika kijiji cha IKuwo, mkuu wa wilaya alipata wasaa wa kutembelea chumba
maalum kilichotengwa kwa ajili ya ushauri nasaha na upimaji, ambapoa alijionea
jinsi shughuli hizo zinaendeshwa kwa watu wanapofika kutaka kupima virusi vya
UKIMWI kwa hiari
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Makete, Ndg. Francis Chaula akiwa Meza Kuu
Akisoma risala ya siku ya UKIMWI duniani mbele ya Mgeni
rasmi na wananchi waliofika kwenye maadhimisho hayo muelimishaji rika Bw.
Boniphace Mbilinyi ambaye anaishi na virusi vya Ukimwi amesema hadi juni mwaka
huu jumla ya watu 246 kutoka kata ya Ikuwo wamepima na kugundulika kuwa wana
maambukizi ya virusi vya UKIMWI na taarifa zao zipo kwenye vituo vinavyotoa
huduma za afya kwa waviu kwani miongoni mwao 112 tayari wanatumia dawa za
kupunguza makali ya VVU (ARV)
Amesema kutokana na kuwepo kwa sababu zinazochangia watu
kupata VVU, bado kata hiyo ina mikakati ya kupambana na ugonjwa huo kwa
kuendelea kutoa elimu, kudhibiti sheria kuhusu unywaji pombe muda wa kazi,
pamoja na kuendelea kuwaelimisha wanaume ili nao wakapime VVU kwa hiari kama
wanavyofanya wanawake
Katika hatua nyingine shirika la SUMASESU limetoa taarifa ya
mapambano dhidi ya UKIMWI na unyanyasaji wa kijinsia katika tarafa ya Ikuwo na
Matamba ambao unatekelezwa na shirika hilo kama njia mojawapo ya kupunguza
maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi kwa jamii hiyo
Wasanii wa Shirika La SUMASESU Wakitoa Burudani Matata kwa Wana- Makete
Akisoma taarifa hiyo kwenye maadhimisho hayo Bi. Anifa
Mwakitalima kutoka SUMASESU amesema katika kipindi cha mwaka mmoja Machi 2012 –
Februari 2013 shirika hilo linatekeleza mradi wa mapambano dhidi ya UKIMWI na
unyanyasaji wa kijinsia ujulikanao kama shule salama unaofadhiliwa na mfuko wa
dharura wa mapambano dhidi ya UKIMWI (RFE) ambapo katika tarafa hizo mbili
mradi unawafikia wanafunzi wa shule za sekondari nne ambazo ni Matamba, Itamba,
Ikuwo na Mlondwe pamoja na wanajamii kutoka vijiji 12 ikiwemo vijiji vitatu
vinavyozunguka kila shule
Amesema pamoja na malengo mengine ya kumjengea uthubutu
mwananfunzi pia inasaidia wanafunzi hao kupambana na vitendo vya unyanyasaji wa
kijinsia pamoja na kujikinga na VVU, ambapo kwa kata ya IKuwo shirika hilo
limewafikia vijana 351 ndani na nje ya shule
Maadhimisho ya siku ya ukimwi duniani kw amwaka huu yalikuwa
na kauli mbiu isemayo “Tanzania bila maambukizi mapya, unyanyapaa na vifo
vitokanavyo na UKIMWI inawezekana”
EmoticonEmoticon