Washiriki kwenye kongamano la kimataifa la kuonesha
mshikamano na wafungwa wa Kipalestina wanaoshikiliwa na utawala wa Kizayuni wa
Israel wameuonya utawala huo ghasibu juu ya ukiukaji wa haki za wafungwa wa
Kipalestina na Kiarabu.
Katika sherehe za ufunguzi wa kongamano hilo, Rais Jalal
Talabani wa Iraq amesisitiza kuwa, hadi sasa hakuna juhudi zozote zinazofanywa
kwa shabaha ya kukomesha machungu na mateso wanayopata wafungwa wa Kipalestina
wanaoshikiliwa kwenye jela za Israel na kufichuliwa siasa zisizo za kibinadamu
zinazofanywa na utawala huo dhidi ya wananchi wa Palestina. Ameongeza kuwa,
kadhia ya Palestina ni kadhia ya ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu tokea miaka 60 iliyopita na kusisitiza kuwa,
kushiriki kwa wingi shakhsia mbalimbali wa kisiasa na kijamii kwenye kongamano
hilo kunaonesha jinsi fikra za waliowengi zinavyochukizwa na siasa za
ukandamizaji za Israel.
Nabil al Arabi, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu
amesema katika kongamano hilo kuwa jinai zinazofanywa na Israel dhidi ya wananchi
wa Palestina hazitafumbiwa macho na kusisitiza kwamba viongozi wa Israel
wanapaswa kufunguliwa mashtaka kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kwa
jinai za kivita walizotenda dhidi ya wananchi wa Palestina. Nabil al Arabi
amesema kuwa, tokea mwaka 2000 hadi sasa wanajeshi wa utawala wa Israel wametia
mbaroni watoto na vijana karibu 2000 wa Kipalestina na jambo hilo linaonesha
ukiukaji wa wazi kabisa wa makubaliano ya kimataifa ya kuwalinda watoto.
Kongamano la kimataifa la kuonesha mshikamano kwa Wapalestina
limeanza leo mjini Baghdad mji mkuu wa Iraq likihudhuriwa na wawakilishi kutoka
nchi 70 duniani.
EmoticonEmoticon