BARAZA la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Bavicha),  limewatumia waraka viongozi
wake wote wa mikoa na wilaya, unaowataka kujiandaa na maandamano ya kushinikiza
viongozi wa juu katika  Wizara ya Elimu
na Mafunzo ya Ufundi, wakiongozwa na Waziri Dk Shukuru Kawambwa, kujiuzulu.
Pamoja na kushinikiza viongozi hao kujiuzulu, Bavicha pia
inaitaka Sserikali  kutangaza matokeo
hayo ni janga la Kitaifa na kuiweka elimu kipaumbele cha kwanza katika bajeti
ya mwaka wa fedha wa 2013/14.
Hatua hiyo imekuja siku kadhaa baada ya kutangazwa kwa
matokeo ya  mtihani wa kidato cha nne,
uliofanyika kote nchini  mwaka jana.
Matokeo hayo 
yalitangazwa na Waziri wa  Elimu
na Mafunzo ya Ufundi,  Dk Kawambwa ambaye
alisema zaidi asilimia 60.6 ya wanafunzi waliofanya mtihani huo wamepata
sifuri.
Waraka huo ambao Mwananchi ilifanikiwa kuupata jana ukiwa
umesainiwa na Katibu Mkuu wa Bavicha,Deogratias Munishi, unawaagiza viongozi hao
kufanya maandalizi  ya haraka ili
kujiandaa na maandamano kama  Dk Kawambwa
hatajiuzulu wiki moja ijayo.
“Kwa waraka huu ndugu viongozi, mnaombwa kufanya yafuatayo;
kuanza maandalizi ya maandamano haya ya kudai elimu bora kwa vijana wa
Tanzania, na pia hatma ya waliofelishwa na Serikali ya CCM kwa kuwasiliana na
hao waliofeli katika maeneo yenu ikiwa ni pamoja na kuwaandikisha sahihi zao
kama sehemu ya wao kuthibitisha kuitaka Serikali iwajibike” ilisema sehemu ya
waraka huo.
Waraka huo pia umewataka viongozi hao kuwahamasisha wananchi
kuunga mkono azimio hilo  
kwa kuwaelimisha vijana na wazazi wao kupitia 
vyombo vya habari, mikutano ya hadhara na vikao vya ndani.
Akizungumzia waraka huo, Munishi alisema huo ni mwanzo wa
utekelezaji wa azimio alilolitoa hivi karibuni la kuaanda maandamano.
MWANANCHI


EmoticonEmoticon