Na: Denis Mlowe - Iringa
Zaidi ya abiria 20 wanusurika kufa katika ajali ya gari aina
ya daladala inayofanya shughuli za kusafirisha abiria kati ya Mkwawa na Kihesa
Kilolo baada ya daladala hiyo kuungua moto na kuteketea kabisa chanzo kikiwa ni
hitilafu katika mfumo wa injini.
Ajali hiyo iliyotokea mida ya saa saba mchana ilihusisha
daladala aina ya kipanya yenye namba T 717 AWK mali ya Ayubu Kabigi ilitokea
katika maeneo ya Mshindo karibu kabisa na kituo cha mafuta cha Sherry na Kanisa
kongwe la Mshindo mkoani hapa.
Shuhuda ya ajali hiyo Anthony Zamilinga amesema kwamba gari
hiyo ilikuwa ikitokea maeneo ya Mwangata ilipofika sehemu ya tukio alimwona
dereva akishuka na kuanza kuchukua mchanga kwa lengo la kupambana na moto
uliokuwa ukianza kuwaka na ulipozidi baadhi ya abiria wakaanza kuruka katika
gari hiyo na kupiga simu katika kikosi cha zima moto kilichofika haraka eneo la
tukio na kuzima katika gari hilo licha ya kuungua na kuteketea kabisa.
Msemaji wa Zimamoto Kaimu Mkuu wa Kituo Sajenti Meja John
Zakaria amesema chanzo cha ajali hiyo hitalafu ya umeme iliyotokea katika gari
hiyo na kuwataka wamiliki wa vyombo vya usafiri kuwa na tabia ya kuwa na vifaa
vya kuzimia moto katika magari yao.
“kikosi cha zimamoto kinatoa elimu kila
mara kuhusu elimu ya kukabiliana na majanga ya moto na kuna namba za simu za
dharura ambazo ziko wazi wakati wote lakini wananchi hawana tabia ya kutoa
taarifa mapema na ndio maana hasara kama hizi zinajitokeza hivyo hatuwezi kuota
kama kuna janga la moto hivyo naomba ushirikiano wa wananchi katika majanga ya
moto kama haya” alisema Sajenti Meja Zakaria
Mmiliki wa dala dala hiyo Ayubu Kabigi amesema kwamba
amepata hasara ya sh milioni 8 kutokana na ajali hiyo na amewashukuru sana
wananchi waliojitokeza kusaidia kuzima gari yake kwani wakati anapigiwa simu
alikuwa anajiandaa na safari ya nje ya mkoa.
“nawashukuru sana wananchi wa
maeneo ya mshindo na kikosi cha zimamoto kuwahi kufika mara baada ya kupewa
habari kuhusu janga hilo licha ya kwamba gari lilikuwa limewaka moto na kuteketea”
alisema Kabigi
EmoticonEmoticon