DAKTARI wa kitengo cha upasuaji katika Hospitali ya Rufaa
Mbeya,Paul Kisabi (32), amefikishwa katika Mahakama ya Mkoa wa Mbeya,
akikabiliwa na mashitaka mawili ya kushawishi na kupokea rushwa ya shilingi
100,000 kutoka kwa mgonjwa aliyefikishwa Hospitalini hapo baada ya kupata
ajali.
Hatua hiyo imekuja baada ya Taasisi ya kuzui na Kuipambana
na rushwa nchini takukuru, kumtia mbaroni daktari huyo juzi kwa tuhuma za
kupokea rushwa ya kiasi hicho cha fedha baada ya kumuwekea mtego.
Daktari huyo Kisabi amepandishwa kizimbani majira ya saa 3:45 na kusomewa mashitaka hayo
mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa wa Mbeya, Fransis Kishenyi,
aliyepangiwa kusikiliza kesi hiyo ambayo imeibua hisia kali kwa wananchi.
Katika kesi hiyo namba 237 ya mwaka 2012, upande wa
mashitaka uliongozwa na waendesha mashita wawili wa Taasisi ya kuzuia na
kupambana na rushwa nchini (TAKUKURU), Joseph Mulebya na Nimrod Mafwele.
Waendesha mashitaka hao walidai kuwa Disemba 19 majira ya asubuhi
akiwa katika sehemu yake ya kazi katika kitengo cha upasuaji, mshitakiwa
alitenda kosa la kwanza la kushawishi rushwa ya shilingi 200,000 kutoka kwa
mgonjwa Meshack Brown, aliyefika hapo kwa lengo la kupatiwa matibabu.
Walisema katika kosa la pili, siku hiyo majira ya saa nane
mchana akiwa katika baa moja iliyojulikana kwa jina la Victoria iliyopo Jijini
hapa, mshitakiwa alitenda kosa lingine la kupokea hongo ya shilingi 100,000,
huku akijua kuwa vitendo vyote hivyo ni kinyume na sheria.
Walisema kuwa kwa mujibu wa sheria za taasisi hiyo, makosa yote
yaliyotendwa na mshitakiwa yanaangukia kwenye kifungu cha 15 ibara ya 1 (a) cha
sheria ya kuzuia rushwa namba 11 ya mwaka 2007.
Kabla kupangwa tarehe ya kutajwa tena kesi hiyo, Wakili wa
mshtakiwa huyo, Ladislaus Rwekaza,aliiomba mahakama impe dhamana mteja wake
akidai kuwa makosa yanayomkabili yanadhaminika.
Hakimu
Kishenyi alikubaliana na maombi ya Wakili Rwekaza kuwa mashtaka yote
yanayomkabili mshtakiwa yanadhaminika na kusema dhamana yake iko wazi.
Alimtaka mshtakiwa huyo kutimiza masharti ya kuwa na mdhamini
mmoja ambaye atasaini mali yenye thamani ya Sh,500,000, na kwamba awe na
utambulisho wa barua kutoka kwa kiongozi wa serikali ya mtaa .
Hata hivyo mahakama ililazimika kuahirishwa kwa muda wa dakika
20 ili kutoa nafasi kwa mdhamini wa mshitakiwa kuleta barua hiyo baada ya kudai
kuwa alikuwa ameisahau kwenye gari lililokuwa nje ya jingo la mahakama.
Baada ya kupokea ombi hilo hakimu Kishenyi aliwahoji waendesha
mashitaka kama wameridhika na hoja, ambao kwa pamoja walikubali kwa
maelezo kuwa dhamana ni haki ya kisheria kwa mshitakiwa hivyo hawakuwa na
pingamizi.
Mshitakiwa aliweza kutimiza masharti ya dhamana hiyo na
hivyo kuachiwa huru hadi januari 7 mwaka 20013 ambapo kesi hiyo itaendelea kusikilizwa
katika mahakama hiyo.
Kwa mujibu wa kumbukumbu za mahama hiyo,
mshitakiwa huyo Daktari Kisabi ni mmoja wa mashahidi wa kesi nyingine
inayoendelea mahakamani hapo ya mtoto Anethi anayedaiwa kuchomwa moto katika
mkono wake, kufungiwa ndani na kulazimishwa kula kinyesi chake na
Shangazi yake.
EmoticonEmoticon