Viongozi 10 wa nchi za eneo la Maziwa Makuu ya Afrika
wanakutana leo mjini Kampala Uganda kwa shabaha ya kuujadili kwa kina mgogoro
unaoendelea kutokota huko mashariki mwa
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Henry Oryem Okello Waziri wa Nchi anayeshughulikia masuala ya
kimataifa wa Uganda amesema kuwa, kikao hicho kitajikita zaidi kutafuta njia za
kuutatua mgogoro huo unaoendelea kuumiza vichwa vya viongozi hao wa Kiafrika na
jumuiya za kimataifa.
Waziri Henry Oryem Okello ameongeza kuwa, kikao cha wakuu
hao wa nchi za eneo watajadili mpango wa kutumwa kikosi cha wanajeshi elfu nne
huko mashariki mwa Kongo kwa lengo la kupambana na waasi wa M23.
Uganda ikiwa
ni mwenyekiti wa mzunguko wa nchi 11 wanachama wa eneo la Maziwa Makuu ya bara la Afrika, hivi
karibuni ilikuwa mwenyeji wa Marais wa Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Kongo, baada ya waasi wa M23 kuuteka mji wa Goma, makao makuu ya jimbo la Kivu
Kaskazini.
EmoticonEmoticon