Marwa Tawfik (Kulia) mmoja wa wajumbe waliowakilisha vyombo
vya habari nchini Misri kuja Tanzania kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii
akifafanua jambo kwa wajumbe wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) na waandishi wa
habari (hawapo pichani) juu ya kile walichojionea walipofanya ziara katika
vivutio mbalimbali vya utalii Tanzania Bara na Zanzibar.Wengine ni baadhi ya
wawakilishi kutoka Misri.
**************************************************
DAR ES SALAAM
DAR ES SALAAM
VYOMBO vya habari nchini Misri vimeahidi kutangaza vivutio
mbalimbali vya utalii vilivyopo nchini katika kuhakikisha Tanzania inapata
watalii wengi zaidi jambo litakaloendelea kudumisha mahusiano mema yaliyopo
kati ya nchi hizo.
Hayo yalisema Dar es Salaam juzi na mmoja wa wawakilishi wa
vyombo vya habari nchini Misri, Marwa Tawfik alipozungumzia ziara waliyofanya
katika vivutio vya utalii nchini ambapo waliahidi kutumia vyombo vyao kutangaza
walivyoviona.
Ujumbe wa watu sita uliowakilisha vyombo mbalimbali vya
habari nchini Misri yakiwemo magazeti na televisheni chini ya Ofisa wa Ubalozi
wa Tanzania nchini humo Jestas Nyamanga walifanya ziara ya siku tano nchini
kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii Tanzania Bara na Visiwani chini ya
uratibu wa Bodi ya Utalii nchini (TTB).
Alisema wanaporudi nchini kwao watakaa na uongozi wa vyombo
vyao na kuangalia jinsi ya kupata vipindi maalumu katika televisheni na makala katika magazeti
jambo litakalowezesha taarifa za utalii za Tanzania kuwafikia watu wengi zaidi
nchini mwao na nchi nyingine za ukanda huo.
Tawfik alisema ana imani ziara hiyo pamoja na kazi
watakayoifanya ya kuvitangaza vivutio husika itasaidia Tanzania kupata watalii
wengi zaidi kutoka nchini mwao na katika nchi za ukanda wa kiarabu. “Tumeona
utajiri wa asili wa ajabu uliopo Tanzania,sisi tunaahidi kutumia vyombo vyetu
kutangaza vivutio hivi katika kuhakikisha watu wengi zaidi wanahamasika kuja
Tanzania na hatimaye kuwaongezea pato lenu kupitia utalii,” alisema Tawfik.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TTB Aloyce Nzuki
alisema ziara hiyo pamoja na nyingine ni muendelezo wa jitihada za bodi hiyo ya
kuhakikisha sekta ya utalii inakua ndani na nje ya nchi.
Alisema ujio wa ujumbe huo kutoka Misri utaongeza idadi ya
watalii kutoka nchi hiyo pamoja na nyingize za ukanda huo ambapo takwimu za
sasa zinaonyesha Tanzania inapata watalii 25,000 kutoka nchi za ukanda huo.
Nzuki alisema pamoja na ujumbe huo kuahidi kutumia vyombo
vyao kutangaza walivyoviona pia bodi hiyo inaendelea na jitihada za kuhakikisha
matangazo ya vivutio vilivyopo nchini yanawekwa katika lugha ya Kiswahili
katika kukuza utalii wa ndani.
“Tumekuwa na jitihada endelevu za kuhakikisha vivutio
tulivyonavyo vinajulikana ulimwenguni kote jambo litakalosaidia kupata watalii
wengi zaidi kutoka nje lakini pia tunaendelea na jitihada za kuhakikisha utalii
wa ndani unakua,” alisema Nzuki.
EmoticonEmoticon