Na: Edson Kamukara
SIKU moja baada ya Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, Rais Jakaya
Kikwete, kuwataka makada wa chama hicho kujibu mapigo ya wapinzani,akidai
wanafanya kazi ya kueneza uongo na kupotosha wananchi, CHADEMA imesema
inamvutia pumzi kabla ya kumjibu.Akihitimisha mkutano mkuu wa CCM mjini Dodoma
juzi usiku, Rais Kikwete aliwataka mawaziri na makada wa chama hicho kufanya
mikutano ya hadhara na kutumia vyombo vya habari kujibu hoja za wapinzani
badala ya kutegemea nguvu za Jeshi la Polisi.
Huku akionekana
kukasirishwa na kasi ya CHADEMA, Rais Kikwete alimtaja wazi wazi Katibu Mkuu wa
chama hicho, Dk. Willibrod Slaa, kuwa aliwahi kumzulia uongo pamoja na mwanaye
Ridhiwani.
“Slaa aliita mkutano akasema mimi, mwanangu Ridhiwani na
Rostam Aziz tulikutana kwenye hoteli moja jijini Mwanza, huku akijua siku
aliyoitaja mi nilikuwa kusini nikiendelea na shughuli zangu,”alisema.
Rais Kikwete alisisitiza kuwa hiyo ndiyo kazi ya upinzani,watu
wazima hovyo,wanasema uongo mbele wananchi na hata wakati mwingine kwenye
vyombo vya habari wakinukuu takwimu za uzushi.
Alipoulizwa jana kuhusu madai hayo ya kueneza uongo kwa
wananchi,Dk.Slaa alicheka kisha akasema:“Tunawatafakari na tutawajibu,ila siyo
leo, wala hatuna haraka.
“Mimi kwa kweli
sikusikiliza hotuba yake, na hata mkutano wa CCM sijaufuatilia, ila kama
Kikwete kasema hayo unayoniuliza, basi tutamjibu kwa utaratibu rasmi wa chama,
leo sisemi kitu.
“Sisi ni watu makini, tunaamini katika kile tunachokisema
wala wasipaniki, tutawajibu.
Maana wanadhani
tunapoteza muda kufuatilia mkutano wao,nilimsikia hata Nape Nnauye akisema juzi
kuwa anajua tumeacha kazi tunawakodolea macho,”alisema.
Dk.Slaa alisema kauli ya Nape ambaye pia ni Katibu wa
Halmashauri Kuu(NEC),Itikadi na Uenezi wa CCM,inachekesha, kwani CCM ya wao
kuacha kazi zao na kuikodolea macho ilikuwa ya zamani si hii ya leo.
Katika kile kinachoonekana kama CHADEMA kuinyima usingizi
serikali na CCM,
Kikwete aliagiza
mawaziri wote kujiwekea utaratibu wa kila mmoja kutoa taarifa za utekelezaji wa
majukumu ya serikali katika vyombo vyote vya habari.
Alisema kwa vile viongozi wa chama na serikali hawajibu
taarifa za upotoshaji zinazotolewa na wapinzani, wananchi wanapozisikia
zikirudiwa rudiwa bila kukanushwa wanaziamini.
EmoticonEmoticon