SERIKALI iko kwenye mpango wa kulifumua na kuliboresha zaidi
Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), ili kuondokana na utegemezi wa shirika
moja linalozalisha, kusambaza na kusafirisha umeme. Waziri wa Nishati na
Madini, Profesa Sospeter Muhongo, alisema hayo jana alipokutana na ujumbe wa
Serikali ya Sweden, uliotembelea nchini ili kupata fursa za uwekezaji katika
sekta ya nishati.
“Kwa kweli hadi hapa tulipofikia Tanesco imejitahidi, lakini
inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwamo ongezeko la mahitaji ya umeme nchini,
ndiyo maana tunaona ni vema kuondokana na utegemezi wa shirika moja kuzalisha,
kusambaza na kusafirisha umeme na kukaribisha wawekezaji wengine,” alisema.
Profesa Muhongo alisema kwa kutambua hali halisi ya umeme
nchini, Serikali imeona umuhimu wa kutafuta namna bora ya ama kuiboresha
Tanesco, ili ifanye kazi yake kwa ufanisi, lakini pia itatoa fursa kwa
wawekezaji wengine kuzalisha umeme na kuusambaza.
“Kwa sasa bado hatujaridhika na idadi ya Watanzania
wanaopata huduma hii, na sote tunajua kuwa maendeleo na kasi ya kukua kwa
uchumi wa nchi yoyote ni upatikanaji wa uhakika wa umeme, sasa tukiendelea na
hali hii ya kuitegemea Serikali katika eneo hili, hatutatimiza malengo yetu,”
alisema.
Alisema tangu Tanesco ianzishwe mwaka 1964 hadi sasa, ni
asilimia 21 pekee ya Watanzania ndio wanapata umeme huku kati yao, asilimia
saba ni wa vijijini na takwimu zinaonesha asilimia 75 ya wananchi wa Tanzania
wanaishi vijijini.
Malengo 2015 Pamoja na Serikali kuanza mchakato wa kufumua
Tanesco kwa kuanza kukusanya maoni ya wadau, Profesa Muhongo alisema kupitia
mipango na miradi iliyopo, Serikali inatarajia ifikapo mwaka 2015, Tanzania iwe
inazalisha megawati 3,000 za umeme.
“Kwa sasa iwapo mitambo yote itawashwa, megawati za umeme
1,438.24 zinazalishwa wakati mahitaji ya juu kabisa ya umeme huo ni megawati za
umeme 850, hata hivyo kuna tatizo kubwa la umeme kupotea njiani ambapo kwa sasa
tunapoteza asilimia 23.4 ya umeme unaozalishwa nchini,” alisema.
Sekta binafsi Ili kufikia malengo hayo, Profesa Muhongo
alisema Serikali imejipanga kufungua ukurasa mpya kwa kushirikiana na nchi na
wawekezaji mbalimbali, wenye nia ya kuwekeza katika sekta ya nishati nchini,
lengo likiwa ni kuhakikisha hali ya upatikanaji wa umeme inaimarika na kufikia
Watanzania wengi.
“Tuache kujidanganya katika hili, Serikali peke yake bila
sekta binafsi haiwezi kuinua sekta ya nishati nchini, tukiisubiri Serikali hii
yenye mapato kidogo, mafanikio katika sekta ya umeme ikiwa ni pamoja na uchumi
kukua, yatachukua muda wa karne nzima kupatikana,” alisisitiza.
Kwa sasa kwa mujibu wa Profesa Muhongo, mapato ya Serikali
kwa mwaka ni takribani dola bilioni 28 za Marekani, ambayo yakigawanywa kwa
kila mwananchi, kila Mtanzania ataambulia dola 600 tu, kiasi ambacho
hakitoshelezi huku kukiwa na mahitaji mengine mengi kama vile, afya, elimu,
miundombinu na maji.
Alisema hata katika bajeti ya Wizara hiyo ya Nishati na
Madini inayotarajiwa kuwasilishwa Mei 22, suala la kuhamasisha uwekezaji katika
sekta hiyo ya umeme, limeelezewa kwa kina ikiwa ni pamoja na kuonesha fursa
zitakazopatikana kwa wawekezaji hao ndani ya sekta hiyo nchini. Misaada Alisema
umefika wakati wa Tanzania kuacha kutegemea misaada na kujikita zaidi katika
eneo la biashara za ubia lengo likiwa ni kujiinua kiuchumi.
“Tumekuwa tukipewa misaada tangu tulipopata uhuru, lakini
hadi leo ni masikini, tuachane na kutegemea misaada haya ni mambo ya kizamani,
kupitia uwekezaji na sisi tuingie kwenye biashara.
Akizungumzia ujumbe huo kutoka Sweden, Profesa Muhongo,
alisema nchi hiyo ambayo ujumbe wake ulifuatana na kampuni zinazojihusisha na
sekta ya nishati, imeonesha nia ya kuwekeza katika maeneo ya uzalishaji umeme,
usambazaji na kuusafirisha.
Waziri wa Viwanda wa Sweden, Gunnar Oom, alisema pamoja na
kwamba malengo ya ziara hiyo nchini ni kuimarisha uhusiano wake na Tanzania,
lakini sababu kubwa ni kuangalia fursa za uwekezaji katika sekta ya nishati.
Alisema tayari wamebaini uwepo wa fursa hizo hasa baada ya
kupewa matatizo na changamoto zinazoikabili sekta ya nishati nchini, likiwamo
eneo la uzalishaji, usambazaji na kuzuia upotevu wa umeme.
EmoticonEmoticon