Na Nathaniel Limu.
Mbunge wa jimbo la
Singida mjini Mh. Mohammed Gullam Dewji ametoa msaada wa pea za
vitenge 7,500 zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 60, kwa
ajili ya kufanikisha maandalizi ya sherehe za CCM kutimiza miaka 36
toka kianzishwe.
Mh. Dewji ametoa msaada
huo mkubwa na wa aina yake, baada ya kuombwa kufanya hivyo na Katibu
wa CCM manispaa ya Singida.
Msaidizi wa mbunge
Dewji, Duda Mughenyi, amesema jumla ya vikundi vya uhamasihaji 112,
vimenufaika na msaada huo wa vitenge.
Amesema pamoja na
vikundi hivyo, pia wajumbe wa halmashauri kuu ya matawi,
wafanyabiashara wa kuku za kienyeji soko kuu, boda boda na taasisi
mbali mbali, watanufaika na msaada huo.
Msaidizi huyo wa
mbunge, amesema kwa hali hiyo, sherehe hii muhimu, ni lazima nayo
ipewe heshima ya aina yake ikiwemo wana- CCM na wapenzi wake,
waonekane tofauti siku hiyo ya sherehe.
Katika hatua nyingine,
Katibu tawi la Ughaugha (CCM), Hamisi Ramadhani, amesema msaada huo
wa vitenge, ni mwendelezo wa misaada mingi ya kimaendeleo anayotoa
mbunge Dewji, jimboni kwake.
“Kwa kweli mimi
binafsi nakiri tu kwamba Dewji anafanya mambo makubwa sana jimboni
kwake. Hivi karibuni ametoa majembe mengi ya kukokotwa na
ng’ombe pamoja na tani nyingi za mbegu ya mbaazi, dengu na
choroko”,amesema.
Ramadhani amesema
msaada huo ambao utamgharimu Dewji zaidi ya shilingi 250 milioni,
unalenga kuwanufaisha wakulima watakaojiunga kwenye vikundi
kujikomboa kiuchumi.
“Kwa sasa baadhi ya
wakazi wa jimbo la Singida mjini wanakabiliwa na upungufu wa
chakula. Hivyo naomba nitumie nafasi hii kumwomba mbunge wetu
Dewji asichoke, atusaidie chakula ili tuweze kunusurika na atharii za
njaa”,amesema.
Kuhusu msaada wa
vitenge, Hamisi amesema msaada huo hauna kabisa harufu ya rushwa, kwa
madai kwamba hauna mambo ya kona kona wala kificho.
Naye mhasibu wa kikundi
cha kijiji cha Misake, Mwajabu Haji, amesema msaada wa sare hizo,
utachochea ari ya kikundi kuongeza bidii katika jukumu lao la
uhamasishaji.