POLISI mkoani Mwanza wamelazimika kutumia risasi za moto na mabomu
ya machozi kuwatawanya waendesha bodaboda waliokuwa wakiwalazimisha
askari wawaachie wenzao waliowakamata kwa makosa mbalimbali.
Wakati hayo yakitokea Mwanza, huko Arusha, madereva teksi
walipandwa na jazba baada ya kuzuka kwa mzozo kati yao na uongozi wa
Hoteli ya Palace kutokana na kile walichoeleza kuwa ni kuondolewa
kinyemela katika eneo lao.
Huko Mwanza, ghasia hizo ziliibuka
wakati polisi wa usalama barabarani na kikosi maalumu cha ukaguzi wa
magari walipofanya doria kukagua leseni na uhalali wa madereva hao
wanaofanya shughuli za kusafirisha abiria.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, vurugu hizo zilianza
saa 2:46 asubuhi baada ya polisi kuwakamata waendesha bodaboda
wapatao 26, ambao walitozwa faini za papo kwa papo kulingana na
makosa yao, huku wengine wakiendelea kushikiliwa.
Hatua hiyo
iliwafanya waanze kujikusanya kutoka sehemu mbalimbali na kuandamana
hadi eneo kulikokuwa limetengwa kwa ukaguzi huo katika Mtaa wa
Mission.
Baada ya kufika eneo hilo, walianza kuwarushia mawe askari
hao, huku baadhi yao wakiendesha pikipiki kuzunguka eneo hilo na
kuzuia magari kupita hali iliyozua tafrani. Baada ya kutokea hivyo,
askari hao walilazimika kuwaita askari wengine ili kuwakabili vijana
hao.
Vurugu hizo zilizodumu kwa saa tatu, zilisababisha kufungwa
kwa barabara iendayo Uwanja wa Ndege na katika eneo la Pasiansi, huku
baadhi ya abiria wakilazimika kuteremka katika daladala na kukimbia
ovyo na wengine kulala katika mifereji ya maji machafu baada ya milio
ya risasi na mabomu ya machozi kuanza kurindima.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ernest Mangu alisema jana
kwamba polisi hao walikuwa katika ukaguzi wa leseni na vifaa vingine
vya usalama kama kofia ngumu ndipo baadhi ya madereva hao wa bodaboda
wakaanza kupinga kukamatwa kwa wenzao na kutozwa faini kutokana na
makosa waliyokuwa nayo.
Mmoja wa waendesha bodaboda ambaye aliomba jina lake
lisiandikwe gazetini alisema kwamba polisi wamekuwa wakiwanyanyasa
kwa kuwachukulia leseni zao, huku wakiwabambikiza makosa mbalimbali
kwa lengo la kujipatia fedha kinyume cha sheria.
Kamanda Mangu
aliwataka waendesha bodaboda hao kutoa taarifa wanaponyanyaswa au
kuombwa rushwa na askari hao.
CHANZO : MWANANCHI