Waafrika wanaoishi ndani na nje ya
mji mkubwa zaidi wa kibiashara nchini India, Mumbai (Bombay), wanalalamika
kuhusu ubaguzi wa rangi na polisi kuwanyanyasa kila mara.
Sambo Davis ni raia wa Nigeria
ambaye amemuoa mwanamke wa kihindi na wanaishi naye mjini Mumbai.
Stakabadhi zake zote ni halali
lakini alikamatwa na polisi hivi karibuni baada ya kushukiwa kuhusika na
bishara za mihadarati.
Yeye pamoja na waafrika wengine 30,
walizuiliwa kwa masaa mengi kabla ya kuachiliwa na kuombwa msamaha.
Lakini siku iliyofuata, bwana Davis
alisema kuwa alishtushwa sana kusoma kwenye magazeti kuwa walikuwa wamekematwa
kwa kuhusika na biashara haramu ya mihadarati.
"polisi
wanatuona sisi kama umbwa," anasema Davis.
Bwana Davis anadai kuwa mara kwa
mara yeye hubaguliwa anapojaribu kukodisha nyumba katika sehemu zenye watu wa
kipato cha kadri.
Hata hivyo yeye ni mmoja wa wale
wenye bahati. Alifanikiwa kupata nyumba nzuri ya kukodisha na yote hayo ni
shukrani kwa mkewe mhindi na pia anamiliki mkahawa mjini Mumbai.
Lakini wenzake kutoka Nigeria,
wanakabiliwa na tatizo la ubaguzi wa rangi. ''Wanapokwenda kutafuta nyumba,
katika maeno fulani, wao huambiwa, 'wewe ni mweusi, wewe ni mnigeria na
hautakiwi hapa'. Huu ni ubaguzi wa rangi.'
Mchezo
wa Paka na Panya
Hakuna idadi kamili ya waafrika
wanaoishi mjini Mumbai, lakini tangu uchumi wa India kuanza kuimarika katika
miaka ya hivi karibuni wengi wamekuja kufanya kazi ndani na karibu na mji huu.
Takwimu zisizo rasmi zinasema kuwa
idadi yao ni zaidi ya watu 5,000.
Wengi wao wanahusika na biashara ya
kuuza nguo nchini Nigeria na katika nchi zengine za kiafrika.
Wengine ni wanafunzi wakiwa kwenye
vyuo vikuu vya kifahari na taasisi zengine za elimu.
Lakini pia kuna mamia ya waafrika,
wengi wao wa Nigeria wanaoishi hapa kama wahamiaji haramu. Aidha wamepoteza
pasi zao za usafiri au muda wao wa kuishi nchini humo umekwisha.
Kila siku watu hawa hujificha ili
wasikamatwe na polisi , kwa sababu ikiwa watakamatwa watatiwa ndani.
Ikeorah Junior kutoka Lagos
anamiliki mkahawa wa vyakula vya kiasili katika eneo moja lenye shughuli nyingi
mjini Mumbai.
"sielewi
kwa nini polisi wanafanya msako wa nyumba hadi nyumba, kuwakamata watu wasio na
stakabadhi zao. Ikiwa hawana stakabadhi halali basi warejeshwe makwao,''
anasema Junior.
Ahmed Javed, mwenye jukumu la
kuhakikisha sheria inafuatwa, katika jimbo la Maharashtra,anasema kuwa hilo sio
rahisi kama inavyodhaniwa.''Wakati mwingine hawana pasi. Kwa hivyo ikiwa uraia
wao haujulikani hawezi kuondolewa nchini humo.''
Mamia ya wahamiaji haramu wanaishi
katika barabara ya Mira mjini Mumbai.
Waafrika wanajulikana kwa majina
mawili hapa India, Negro au kaalia.
"sisi huwaita Negro kwa sababu
ni weusi na wanaogopesha sana,'' alisema mwanamke mmoja.
''Hawawezi kupata nyumba mjini
Mumbai,ndio maana wanaishi katika barabara hii ya Mira nje kidogo ya Mumbai.
Kwa nini? Kwa sababu ya wanavyoendesha maisha yao. Wao huuza madawa ya kulevya
na wanajihusisha na vitendo haramu. Hahawezi kuaminiwa,'' alisema mwanaume
mmoja mkongwe.
Aibu
kubwa
Licha ya hali hii, Sheeba Rani
aliolewa na Sambo Davis miaka minne iliyopita na wana watoto wawili.
Bi Davis anasema kuwa wazazi wake ni
wakristo na waliwatakia kila la kheri katika ndoa yao kwa sababu wanaamini kuwa
ndoa yao ni mapenzi ya Mungu.
Lakini anasema kuwa marafiki zake,
jamaa zake na jamii kwa ujumla walimtenga tangu alipooa.
Bi Davis anasema kuwa tabia ya watu
wake kwa waafrika weusi inamtia aibu sana
"siku ambazo nilikuwa natembea
naye tukienda zetu madukani, nilimtaka saa zote kunishika mkono. Lakini watu
walipotuona, walidhani natoka kwa familia mbaya au hata kuwa mimi ni kahaba.''
Zamani kidogo hakujua kwa nini watu
weusi wanabaguliwa sana lakini siku hizi anaelewa.
"kwa sababu watu wetu wanapenda
ngozi nyeupe. Ikiwa ningeolewa na mzungu, watu wangenipenda sana na
ningekubaliwa zaidi na jamii.''
Bwana Davis anasema anaamii kuwa
anabaguliwa tu kwa sababu yeye ni mweusi. Kwa sababu anatoka Afrika na kuwa
yeye ni mnigeria. Nadhani wahindi wanatuona sisi kama sio watu kama wao.
CHANZO: BBC