WAKALA Maarufa wa M-pesa Vodacom na
Mkazi wa Kibaoni mjini Singida Mashaka Omari Makiya (30) amejipiga risasi
kichwani na kusababisha kifo chake papo hapo.
Mashaka maarufu kwa jina la
Mashakom, amejipiga risasi kwa kutumia bastola yake aina ya ‘silencer’ usiku wa
Desemba 27 mwaka huu, nyumbani kwake Ipembe mjini hapa.
Shuhuda wa tukio hilo,Shija John
amesema Desemba 28 mwaka huu saa saba mchana askari polisi walifika nyumbani
kwa marehemu iliyopo mkabala na nyumba ya kulala wageni ya Meatu eneo la
Ipembe.
Amesema askari polisi hao waliingia
chumbani kwa Mashaka ambapo walikuta mwili wa mfanyabiashara huyo ukiwa
sakafuni.Pia walikuta bastola yake ikiwa pembeni mwa mwili huo pamoja na simu
zake tatu.
“Taarifa nilizonazo ni kwamba
mfanyakazi wa Mashaka aligundua tukio hilo na kisha alitoa taarifa kituo kikuu
cha kati cha polisi na askari walifika mara moja”,amesema.
Katika hatua nyingine, mwandishi wa
habari hizi aliweza kufika kwenye moja ya maduka yake matatu ya M-pesa na
kushuhudia ujumbe wa maandishi ulioachwa na Mashaka ndani ya gari lake jeusi.
Pamoja na askari polisi kukataa
kutoa kibali kwa waandishi habari kusoma
ujumbe huo au kuupiga picha,watu waliobahatika kuusoma ukiwa ndani ya gari
wamedai kuwa marehemu amemhusisha na kifo chake mfanyabiashara mmoja (jina
tunalo) aliyekuwa na mahusiano ya karibu ya kibiashara pia marehemu Mashaka
ameagiza kuwa nyumba na fedha zake wapewe wadogo zake.
Kifo cha Mashaka kimezua hofu kubwa
na kazi ya uwakala wa M-pesa kwa madai kwamba katika miaka michache waliokuwa
wafanyabiasha wa uwakala huo,Tembs na Rweyemamu wote wamepoteza maisha kwa
kupigwa risasi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida,
SACP Geofrey Kamwela amesema bado hajapata taarifa hizo na ameahidi
kulifuatilia na kutoa habari ili jamii iweze kujua kilichojiri.