Chama cha Wananchi (CUF) kimetangaza
wagombea wa nafasi ya ubunge na uwakilishi kwa majimbo 54 ya uchaguzi kwa
nafasi na uwakilishi na majimbo 50 kwa nafasi ya ubunge huku kikimtema kigogo
wake, Muhammed Habibu Mnyaa (pichani), baada ya jimbo lake la Mkanyageni
kufutwa na Tume ya Uchaguzi (Zec).
Mkurugenzi wa uchaguzi wa
chama hicho, Omar Ali Shehe, alisema baada ya Zec kufanya mabadiliko ya
mgawanyo wa majimbo na kuongeza majimbo manne mapya, chama hicho kililazimika
kufanya mabadiliko ya wagombea wa majimbo.
Alisema baadhi ya wagombea
waliogombea majimbo ya zamani na sasa yamebadilishwa majina wamewapa majimbo
hayo yaliobadilishwa majina na kuwaongeza wagombea wanne kwa majimbo mapya kwa
nafasi za uwakilishi.
Mnyaa alikataliwa na wananchi
katika kura za maoni, lakini baadaye Baraza Kuu la Uongozi likapitisha jina
lake kugombea nafasi hiyo, hatua iliyoibua malalamiko kutoka kwa wanachama wa
CUF kwa madai ya kuwa hakuwa chaguo lao.
Baraza Kuu la CUF lilirejesha
jina la Mnyaa kabla ya Zec kutoa ripoti ya mapitio na mgawanyo wa majimbo na
baada ya kumaliza kazi hiyo tume ililifuta jimbo la Mkanyageni alilokuwa
akiliongoza.
Shehe alisema jana kuwa
utaratibu uliotumika katika kuwapata wagombea wa majimbo mapya wamefuata katiba
ya chama ambayo inaruhusu kufanya mabadiliko katika hali ya dharura.
Aidha, CUF imemrejesha Naibu
Naziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati, Haji Makame Mwadini ambaye alibwagwa
katika kura za maoni kutetea nafasi yake ya uwakilishi kwa jimbo la
Nungwi na jina lake halikurejeshwa na Baraza Kuu la chama hicho, lakini sasa
amepewa kugombea jimbo la Kijini.
Waliobadilishwa majimbo baada
ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) kutaja majina mapya kwa baadhi ya majimbo ni
Mji Mkongwe, Ismail Jussa Ladhu (sasa Malindi) wakati ni Ali Saleh aliyekuwa
anagombea ubunge Mji Mkongwe (sasa Malindi).
Wengine ni mwakilishi wa jimbo la
Mtoni, Nassor Ahmed Mazrui amepelekwa jimbo la Mtopepo, Mansour Yussuf
Himid uwakilishi jimbo la Chukwani badala ya Kiembe Samaki na Abdillahi Jihadi
Hassan uwakilishi jimbo la Mwanakwerekwe badala ya Magogoni