Katika siku za hivi karibuni, kumejitokeza taarifa zenye tuhuma kadhaa dhidi ya Idara ya Usalama wa Taifa.
Taarifa
hizo zimekuwa zikitolewa kwenye vyombo vya habari zikiihusisha Idara
hii na matukio ambayo yanaidhalilisha na kuzua maswali mengi kwa
wananchi. Kati ya tuhuma hizo ni tukio la kutekwa kwa Dr. STEPHEN
ULIMBOKA, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari na madai ya kufanywa kwa
mipango ya kuwadhuru baadhi ya Viongozi wa Vyama vya Upinzani.
Gazeti
moja la kila wiki limekuwa likurudia tuhuma hizo mara kwa mara kwa
madai kwamba ni habari za uchunguzi na kuihusisha Idara.
Idara
inataka kuwahakikishia wananchi kwamba taarifa hizo ni za UZUSHI NA
UONGO ambazo zina nia ya kuharibu jina na sifa ya Idara. Taarifa hizo
zimekuwa zikiunganishaunganisha vipande vya taarifa mbalimbali ili
kukidhi malengo yaliyokusudiwa na wanaolitumia gazeti hilo. Idara
haikuhusika wala haihusiki na matukio yoyote yaliyotajwa katika tuhuma
hizo. Hivyo tunawaomba wananchi wazipuuze taarifa hizo.
Matukio
yaliyotajwa katika tuhuma hizo yanachunguzwa na Jeshi la Polisi
ambacho ndicho Chombo Chenye Dhamana, na kwa Maslahi ya Taifa si vizuri
kuachia upotoshaji huo uendelee.
Aidha, tunapenda
kuwahakikishia Watanzania kuwa uzushi na tuhuma zinazotolewa dhidi ya
Idara hazitatuvunja moyo bali zitatuunganisha na hivyo kutuimarisha
katika azma yetu ya kuhakikisha nchi yetu inaendelea kubaki salama kwa
kushirikiana na wanachi na Vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama.
Imetolewa na Idara ya Usalama wa Taifa,
Makao Makuu,
DAR ES SALAAM