Imeandikwa na Theopista Nsanzugwanko, Halima Mlacha na Lucy
Lyatuu
BAADA ya uchunguzi wa awali wa madaktari katika Hospitali ya
Muhimbili Dar es Salaam kubaini kwamba Mhariri Mtendaji wa New Habari
Corporation, Absalom Kibanda mbali na kujeruhiwa kichwani, kung’olewa meno,
kucha na kukatwa kidole, zimebainika athari nyingine kwake.
Uchunguzi uliofanywa jana na madaktari wa Hospitali ya
Milpark, Johannesburg, Afrika Kusini alikolazwa, umeonesha kuwa mbali na hayo,
fizi kati ya pua na kinywa imekatika kutokana na nguvu na nyenzo walizotumia
watesaji wake kumng’oa meno na kumsababishia maumivu makali.
Taarifa iliyotolewa jana na Katibu wa Jukwaa la Wahariri
Tanzania (TEF), Neville Meena akikariri taarifa za Johannesburg, ilisema
Kibanda ambaye pia ni Mwenyekiti wa TEF, meno yake sita yamelegea.
Ilisema tangu awasili jana Milpark, amekuwa akiendelea na
matibabu kwa maana ya kufanyiwa vipimo vikiwamo vya CT Scan na X Ray hasa
kichwani na sehemu nyingine za mwili ambazo zilipata majeraha.
“Baada ya kukamilika kwa uchunguzi huo, jopo la madaktari
wenye ujuzi wa aina tofauti, walikuwa wakitarajiwa kukutana ili kusoma taarifa
ya matokeo ya uchunguzi huo, ili kutafsiri maana ya matokeo hayo, kisha kutoa
mwelekeo wa nini kinafuata au aina ya tiba anayopaswa kupata,” ilisema taarifa.
Jana uongozi wa Jukwaa la Habari za Kiuchunguzi la Afrika
Kusini ulimtembelea Kibanda hospitalini Milpark na kueleza masikitiko yake
kuhusu yaliyomkuta.
Waliahidi kushirikiana na taasisi za kihabari za Tanzania,
kuchunguza tukio hilo kwa lengo la kupata majawabu ya nini kilichojiri na
sababu za unyama huo.
Akizungumza na gazeti hili jana mchana, mke wa Kibanda,
Angela Semaya alisema kwa mujibu wa muuguzi anayemshughulikia mumewe, walikuwa
wakimsubiri daktari na wataalamu wengine ili kusoma vipimo kujua kiwango cha
athari.
Alisema baada ya kusoma vipimo na kujua alivyoathirika
ataanza matibabu ya jumla. Semaya alisema kwa sasa mumewe anaendelea vizuri
kwani ana kumbukumbu zote, lakini mara nyingine analalamika maumivu sehemu
alizojeruhiwa.
Kituo chalaani Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) kimesema
kimepokea kwa mshituko na mshangao taarifa za kuvamiwa na kushambuliwa kwa
Kibanda na kulaani wahusika na tukio hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana,
Mwenyekiti wa Kituo hicho, James Mbatia, aliliita tukio hilo kuwa ni ovu na la
kiharamia lisilopaswa kuvumiliwa.
“Kikao chetu cha TCD kinatoa pole nyingi kwa ndugu wa
Kibanda na kumwombea heri aweze kupona haraka ili aendelee na majukumu yake.
Lakini pia tunalaani kwa nguvu zote tukio hili,” alisema Mbatia.
Alisema kituo hicho kinavitaka vyombo vya ulinzi na usalama
kufanya uchunguzi wa kina wa tukio hilo kwa haraka ili wahusika wakamatwe na
sheria ichukue mkondo wake.
“Lakini tunasisitiza kuwa Serikali iwe makini zaidi
kukomesha matukio ya namna hii ambayo yameanza kukithiri nchini, kwani
yanajenga wasiwasi, chuki, uhasama na hasira miongoni mwa raia wa Tanzania na
kuhatarisha usalama wa amani ya nchi yetu,” alisema.
Warioba azungumzia Naye Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba, Jaji mstaafu Joseph Warioba alisema ni tukio linaloleta wasiwasi katika
jamii na kutaka wananchi kushirikiana na Polisi katika kuyatokomeza.
Alisema tukio hilo linaonesha kuwa si la kijambazi ni kisasi
cha kukomoana na ambayo yanaweza kuleta hatari kubwa katika jamii. “Tukio hili
si la ujambazi ni la kulipiza kisasi cha kukomoana … yanatakiwa kudhibitiwa,
kwani tofauti na hivyo yatakuwa hatari sana katika jamii,” alisema Warioba.
Kibanda alivamiwa saa sita usiku wa kuamkia juzi, nje ya
lango la kuingilia nyumbani kwake wakati akirejea nyumbani akitoka kazini na
alitobolewa jicho, kung’olewa meno, kukatwa kidole cha mkono, kupigwa mapanga
mguuni, kupigwa na nondo kichwani na mikononi ambapo wavamizi hawakuchukua
chochote.
Kabla ya kusafirishwa nchini Afrika Kusini alikuwa akipatiwa
matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na Taasisi ya Mifupa Muhimbili
(MOI).