MHUDUMU wa
nyumba ya kupumzikia wageni wa Kanisa la KKKT Dayosisi ya Mashariki ya Ziwa
Victoria, jijijini hapa, amejeruhiwa vibaya baada ya kulipukiwa na bomu
lililokuwa limewekwa kwenye korido la nyumba hiyo.
Tukio
hilo lilitokea jana (Jumatatu), kati ya saa 1:45 na saa 2:20 usiku, katika eneo
la Makongoro wilayani Ilemela wakati mhudumu huyo Bernadetha Alfred (25)
alipofungua kifurushi cha mzigo alichodhani kimesahaulika kwenye eneo hilo,
kabla ya kumlipukia.
Kwa
mujibu wa Katibu wa Dayosisi hiyo, Mollel Rogart, kifurushi hicho kilichokuwa
kwenye mfuko mweusi wa nailoni, kilikuwa juu ya kreti (tupu) za soda, karibu na
eneo la kulia chakula lililopo katika nyumba hiyo.
“Ule
mfuko ulikaa pale siku tatu ndiyo usiku huo mhudumu wetu akakichukua
kukiangalia akidhani ni mzigo wa mtu umesahaulika.” Alieleza Katibu huyo na
kudai kuwa kifurushi hicho kilimlipukia mara tu alipokifungua na kujeruhi
vibaya katika sehemu mbalimbali za mwili.
“Bernadetha
kajeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili ikiwemo miguuni na usoni na siwezi kusema
kwamba chanzo cha mlipuko huo ni mambo ya kidini japo ulinzi wetu haukuwa mkali
kiasi cha kudhibiti watu walioingia na vitu.” Alisema
Kamanda
wa polisi mkoani Mwanza, Valentino Mlowola akithibitisha tukio hilo, alisema kwamba
uchunguzi wa awali uliofanywa na kikosi maalum kutoka Dar es salaam umebaini
kuwa bomu hilo limetengenezwa kienyeji.
“Bado
tunaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ili tubaini ni nani kafanya ili kama ni
mtu au kikundi kimehusika tuchukue hatua haraka. Natoa wito kwa wananchi
kutochukua vitu ambavyo hawa uhakika navyo, wanapoona vitu vya aina hiyo, watoe
taarifa kwetu.” Alisema Kamanda Mulowola.
Mlowola
alieleza kuwa, Bernadetha aliyejeruhiwa vibaya katika sehemu mbalimbali za
mwili, alikimbizwa katika Hospitali ya rufaa ya Bugando ambako anaendelea na
matibabu.
Kamanda
huyo alieleza kwamba, mabomu (yakiwemo ya kienyeji) yako katika mifumo
mbalimbali hivyo wananchi hususan wahudumu wa sehemu za mikusanyiko wawe na
tahadhari na vitu vinavyoonekana kusahaulika na wasisite kuwajulisha polisi
vinapoonekana hivyo.
Mlipuko
huo uliozusha hofu kwa waumini mbalimbali wakiwemo wa Kanisa hilo, umetokea
ikiwa ni wiki moja baada ya maadhimisho ya ‘Huduma ya Mtoto’ kwa makanisa
mbalimbali ya Kikristu jijini hapa yaliyofanyika kwenye kanisa hilo,
yakitanguliwa na maandamano kutoka uwanja wa furahisha hadi KKKT.