REPIN ROCK CITY

REPIN ROCK CITY

TUMA TRACK YAKO

LOWASA AWAUNGA MKONO CHADEMA

2:54:00 AM 1 Comment



Ni kuhusu elimu bure hadi sekondari, asema iwe moja ya ajenda za ccm 2015

WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amesema wakati umefika kwa sasa hapa nchini elimu ya Sekondari iwe elimu bure na kumwondolea mwananchi wa kawaida mzigo wa kubeba gharama za elimu hiyo.
Lowassa akizungumza jana mjini Babati alisema, mjadala kuhusu elimu kutolewa bure hadi sekondari haukwepeki, hivyo kuwataka wadau wa elimu kuanza sasa kujadili suala hilo na kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinapaswa kulifanya hilo kuwa moja ya ajenda zake katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Alisema elimu ya sekondari ikifanywa bure, itakuwa ni fursa kwa kila mtoto wa Kitanzania kuipata. Hatua ambayo itaongeza weledi na uelewa wa mambo mengi katika jamii.

“Ninasema sasa wakati umefika elimu ya sekondari kuwa kama elimu ya msingi kwa watoto kusoma bure kuanzia kidato cha kwanza hadi kidato cha nne,” alisisitiza Lowassa ambaye ni Mbunge wa Monduli (CCM).

Kwa kauli hiyo, Lowassa ni kama ameunga mkono Sera ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambao waliingia katika mgogoro na CCM kuhusu elimu kutolewa bure wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2010.
Chadema wamekuwa wakisisitiza kwamba elimu bure inawezekana hadi ngazi ya sekondari, lakini wakati wote CCM wamekuwa wakisema kuwa suala hilo haliwezekani na kwamba kauli za aina hiyo ni kuwahadaa wananchi.

Katika Uchaguzi Mkuu wa 2010, aliyekuwa mgombea wa urais kupitia Chadema, Dk Willibrod Slaa alitumia sera ya elimu bure kuanzia chekechea hadi sekondari kama kete ya kusaka ushindi, huku akisema chama chake kingetenga asilimia 35 ya bajeti kwa ajili ya kuboresha elimu na kutoa elimu bure.

Hata hivyo, aliyekuwa mgombea wa CCM na baadaye kupata ushindi, Rais Rais Jakaya Kikwete alikuwa akiwatahadharisha wapigakura kuwa kwamba ahadi ya Chadema ni hewa na kwamba hilo lisingewezekana.
Mvutano huo uliwaingiza makada wengine ambao ni Katibu Mkuu wa CCM, 

Abdulrahman Kinana ambaye wakati huo alikuwa Meneja Kampeni wa CCM na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta na kwa upande wa Chadema, Dk Kitila Mkumbo naye alijitokeza kutetea sera ya chama chake.
Katika mkutano wa kampeni za CCM uliofanyika Novemba 10, 2010 katika Kata ya Mchangimbore katika Jimbo la Peramiho mkoani Ruvuma, Rais Kikwete alisema “Serikali haiwezi kutoa huduma za jamii bure” na kwamba lazima wananchi wachangie.
“Nimebahatika kukaa serikalini muda mrefu hiyo sera ya bure tulijaribu na ikatushinda na wakati huo Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, tulikaa naye tukaona hilo haliwezekani tukaamua tubadilishe sasa nawashangaa wenzetu wanawadanganya eti watatoa bure.”

Kwa upande wake Dk Slaa akiwa mjini Arusha katika moja ya mikutano yake alisema kwamba CCM walikuwa wakipinga sera ya elimu bure hadi sekondari kutokana na kulea ubadhirifu na kuthamini anasa kuliko maendeleo kwa wananchi.
Kauli ya Lowassa
Jana akizungumza muda mfupi kabla ya kuanza kuendesha harambee ya ujenzi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT) Usharika wa Babati, Lowassa alisema wakati umefika kwa kila Mtanzania kuzungumzia suala hilo bila ya woga.

CHANZO : MWANANCHI

WATU 7 WAUAWA NA WENGINE 30 KUJERUHIWA NCHINI KENYA

12:31:00 AM Add Comment
NAIROBI, Kenya


Watu wasiopungua 7 wameuawa na wengine 30 kujeruhiwa katika mlipuko uliotokea kwenye gari la abiria maarufu kwa jina la  'matatu' mjini Nairobi, Kenya. 

Polisi ya Nairobi imetangaza kuwa, mlipuko huo umetokea kwenye eneo la Eastleigh ambalo linakaliwa na Wakenya wenye asili ya Kisomali. Hadi sasa haijafahamika ni kikundi gani ambacho kilitekeleza shambulio hilo la bomu la kutegwa ndani ya basi la abiria. 

Kwa upande mwengine, watu wasiopungua 18 wamejeruhiwa  kufuatia machafuko yaliyotokea muda mchache baada ya kutokea mlipuko wa basi la abiria la 'matatu' mjini Nairobi. Taarifa zinasema kuwa, wengi kati ya majeruhi hao walikuwa wamechomwa visu na wengine wakiwa na majeraha yaliyotokana na kupigwa mawe. 

Maduka kadhaa ambayo ni ya Wasomali yalilengwa katika mashambulio hayo ambapo vijana wa Eastleigh walikuwa wakiwatuhumu Wasomali hao kwamba, ndio waliohusika na mlipuko wa basi la abiria la 'matatu'.

WAPAALESTINA 23 WAUAWA TENA KATIKA MAPSHAMBULIZI HUKO GAZA

12:23:00 AM Add Comment
GAZA


Wapalestina wasiopungua 23 wameuwawa jana katika Ukanda wa Gaza huku mapambano makali kati ya Israel na wanamgambo wa kundi la Hamas yakizidi kupamba moto. 

Wizara ya afya ya Gaza inayoendeshwa na Hamas imesema wengi wao walikuwa watoto. Idadi ya watu waliouwawa katika mzozo huo uliodumu siku tano sasa, imefikia 69. Israel imesema mfumo wake dhidi ya makombora umeyaangusha maroketi mawili yaliyovurumishwa kutoka Ukanda wa Gaza katika anga ya mji wa Tel Aviv. 

Waisraeli 3 wameshauwawa na maroketi kutoka Gaza tangu Jumatano iliyopita. Ongezeko la machafuko linakuja huku waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu akionya kwamba nchi hiyo iko tayari kuitanua harakati yake ya kijeshi. 

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon jana ameitaka Israel na Hamas kushirikiana na Misri kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano.

MZOZO WA TANZANIA NA MALAWI KUPATA MPATANISHI...

12:06:00 AM Add Comment
DAR ES SALAAM, Tanzania


Serikali za Tanzania na Malawi zimefikia makubaliano ya kumtafuta mpatanishi wa kimataifa atakayetatua hitilafu za mpaka wa majini kati ya nchi hizo mbili. 

Bernard Membe Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Tanzania ameyasema hayo mjini Dar es Salaam alipokutana na mwenzake Ephrahim Muganda Chiume wa Malawi na kuongeza kuwa, pande hizo mbili zimechukua uamuzi wa pamoja wa kuupeleka mgogoro huo kwa jopo la maraisi wastaafu wa Afrika linaloongozwa na Joaquim Chissano Rais wa zamani wa Msumbiji ambalo linashughulikia kutatua hitilafu na migogoro mbalimbali barani  Afrika. 

Pande hizo mbili zimeafikiana kwamba, iwapo hazitaridhishwa na maamuzi ya upatanishi huo, zitalazimika kuwasilisha hitilafu zao kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ. Malawi inadai kwamba mpaka wa nchi hizo mbili upo kwenye ufukwe wa Tanzania kwa maana kwamba nchi hiyo haina haki ya kutumia maji ya ziwa hilo ambalo linahesabiwa kuwa ni la tatu kwa ukubwa barani Afrika. 

Hii ni katika hali ambayo, Tanzania nayo inadai kuwa mpaka wa nchi hizo mbili uko katikati ya maji ya ziwa Nyasa. Mgogoro kati ya Tanzania na Malawi ulianza mwezi Julai mwaka huu baada ya Malawi kuanza kufanya utafiti wa mafuta katika eneo la Tanzania, hali ambayo ilisababisha serikali hizo mbili kuanza kulumbana. Inasemekana kuwa, chini ya maji ya ziwa hilo kuna utajiri mkubwa wa mafuta na gesi.

MNADA BANNER