RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewataka viongozi wa dini na wanasiasa kupima kauli na vitendo
vyao ili kuepusha kuligawa taifa kwa misingi ya imani za dini na itikadi za
siasa, kama ilivyotaka kujitokeza mwaka 2012.
Katika
salamu zake za Mwaka Mpya kwa Taifa juzi, Rais Kikwete alisema kwa mara ya
kwanza mwaka 2012, Tanzania ilifikishwa
kwenye hatari ya kutokea mgawanyiko wa Watanzania au hata mapigano kwa misingi
ya dini zao.
“Nimeshalisemea
jambo hili siku za nyuma na napenda kurudia leo kuwasihi Watanzania wenzangu
kupima athari za kauli zetu na matendo yetu kwa mustakabali wa jamii yetu, nchi
yetu na watu wake,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:
“Viongozi
wa dini, waumini na viongozi wa siasa na wafuasi wao wanao wajibu maalumu wa
kuhakikisha kuwa Watanzania wanaendelea kuishi kwa upendo, amani na ushirikiano
bila kujali tofauti ya dini zao, makabila yao, rangi zao au maeneo watokako.”
Ingawa
Rais Kikwete hakutaja mambo yaliyotaka kuligawa taifa mwaka jana, mwaka huo
ulikumbwa na matukio kadhaa yaliyohusishwa na imani za kidini ikiwamo uchomaji
wa makanisa katika Miji ya Zanzibar na Dar es Salaam.
Matukio
mengine ambayo baadhi ya watu waliyahusisha na imani za dini ni vurugu
zilizofanywa na wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa Kikundi cha Waislamu wa Taasisi
za Jumuiya ya Kiislamu Tanzania ambazo ni pamoja na kuvamia Ofisi za Makao
Makuu ya Wizara ya Mambo ya Ndani, Dar es Salaam na uvamizi wa maeneo ya wazi
eneo la Temeke. Hata hivyo, watu kadhaa walikamatwa na kufunguliwa mashtaka
katika mahakama mbalimbali nchini kwa tuhuma za ama kushiriki au kuongoza
vurugu hizo.