Mkuu wa mkoa wa Singida Dk.Parseko Kone akizungumza na
baadhi ya walimu wa shule ya sekondari Mwanzi Manyoni mjini.Dk.Kone
hakufurahishwa na hali duni ya ofisi ya mkuu wa shule hiyo wakati shule ikiwa
na akiba ya zaidi ya shilingi milioni sita
Na Nathaniel Limu.
Mkuu wa mkoa wa
Singida Dkt. Parseko Kone amemwagiza mkurugenzi mtenadaji wa halmashauri ya
wilaya ya Manyoni, achague walimu wakuu wanne wa shule za msingi na wakuu wa
shule za sekondari wanne, awapeleke shule ya msingi mchanganyiko Ikungi, ili
wakajifunze juu ya matumizi bora ya fedha za umma.
Akizungumza na walimu wa shule ya sekondari ya Mwanzi
iliyopo mjini Manyoni pamoja na viongozi wa wilaya ya Manyoni Dkt. Kone amesema
shule ya msingi mchanganyiko Ikungi wilaya ya Ikungi,ni shule ya mfano mkoani
Singida kwa matumizi mazuri ya fedha za uuma.
Amesema Ofisi ya mkuu wa shule hiyo ni nzuri mno, pengine si
rahisi kuifananisha na ofisi nyingi za wakuu wa wilaya. Ina samani za kisasa,
tv, kompyuta, internet, jokofu na makochi ya hali ya juu na kuwa Ofisi kama ile
inavutia na inachangia mhusika kubaki ofisini kipindi chote cha kazi.
Akifafanua zaidi, amesema majengo ya shule ya msingi
mchanganyiko Ikungi pamoja na ujenzi wa uzio wa ukuta, yamekarabatiwa/kujengwa
yana ubora unaofanana na thamani ya fedha zilizotumika.
Dkt. Kone amesema walimu wakuu wa shule za msingi na wakuu
wa shule za sekondari, hawana budi kufika kwenye shule hiyo ili kujifunza
mwenzao Olivary Kamilly (mwalimu mkuu wa shule ya msingi mchanganyiko Ikungi)
anavyutumia fedha za umma vizuri.
Mkuu huyo wa mkoa, ametoa agizo hilo, baada ya
kutokuridhishwa na hali duni ya ofisi ya mkuu wa shule ya sekondari Mwanzi
mjini Manyoni, wakati shule hiyo benki ina zaidi ya shilingi milioni sita
ambazo zimekaa kwa muda mrefu bila kutumiwa.
Katika hatua nyingine, Dkt. Kone amewaagiza watendaji wa
halmashauri za wilaya na Manispaa, kujenga utamaduni wa kutembelea miradi mara
kwa mara, ili miradi yote ya maendeleo iweze kutekelezwa kwa ubora unaofanana
na fedha zilizotumika.
Amesema katika ziara yake wilayani Manyoni, amebaini baadhi
ya miradi imetekelezwa chini ya kiwango na kitendo hicho kimechangiwa na
viongozi kutokwenda vijijini kutembelea
miradi.
“Acheni tabia ya kukaa maofisini, jengeni utamaduni wa
kusimamia kikamilifu miradi ya maendeleo, ili iwe na ubora unakusudiwa uweze
kufikiwa”alisema Dk.Kone.
Aidha, amewataka kutunza vizuri miradi iliyomalizika na ile
inayohitaji ukarabati, ifanyiwe ukarabati unaofanana na thamani ya fedha
zitakazotumika.