Dk Hussein Mwinyi, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii |
Utangulizi
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inapenda kutoa taarifa kwa
umma, kuhusu tetesi zilizokuwa zimeenea hapa nchini kutoka kwenye vyombo mbali
mbali vya habari kuhusu kuwepo kwa mgonjwa wa Ebola,wilayani Karagwe mkoa
wa Kagera.
Mnamo tarehe 3 Agosti 2012, Wizara ya Afya na Ustawi Wa
Jamii ilipokea taarifa kutoka kwa mganga mkuu wa wilaya ya Karagwe ya kuwepo
kwa mgonjwa aliyekuwa anahisiwa kuwa na dalili za ugonjwa wa Ebola, katika
hospitali ya Wilaya ya Nyakahanga.
Aidha,taarifa hiyo
ilibainisha kuwa mgonjwa huyo alikuwa ni mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka
(6|) kutoka katika kijiji cha Nyakatundu
wilayani Karagwe. Mgonjwa huyu alikuwa na dalili za homa kali, kulegea, kutokwa
damu puani, kutapika damu, na kukojoa
damu.
Maelezo kutoka kwa mama mzazi zilieleza kuwa mtoto huyu
alianza kuugua kuanzia tarehe 30 Agosti 2012, ambapo alipatiwa dawa ya Septrin
baada ya hospitali binafsi kuonyesha kuwa ana
ugonjwa wa“Typhoid”.
Uchunguzi wa awali katika hospitali ya Nyakahanga ulionyesha
kuwa mtoto huyu alikuwa anasumbuliwa na
uambukizo kwenye haja ndogo (Urinary Tract Infection).Vile vile alifanyiwa
uchunguzi wa kimaabara na Vipimo vya malaria, Hepatitis na Typhoid
havikuonyesha kuwepo kwa magonjwa haya.
Hospitali inaendelea kumpatia matibabu mtoto huyu na imewaweka mgonjwa na mama
yake anayemtunza kwenye chumba maalum (Isolatiom room) kwa ajili ya uangalizi zaidi.
Aidha mnamo tarehe 4 Agosti 2012, timu za wataalamu kutoka
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na timu ya mkoa wa Kagera
imeweza kufika na kumfanyia uchunguzi wa kina pamoja na kuchukua sampuli za
damu kwa ajili ya uchunguzi zaidi katika maabara ya Taifa ya uchunguzi wa magonjwa
na Maabara za nje ya nchi, ili kubaini kama ameathirika na ugonjwa wa Ebola.
Timu hiyo ya wataalamu imetoa taarifa kuwa hali ya mgonjwa
huyu kwa sasa imeimarika ikiwa pamoja na kutokuwa na homa, kutapika na kukojoa
damu kumekoma pia, uchunguzi uliofanywa kwa mama wa mtoto umeonyesha kuwa hana
dalili zozote za ugonjwa wa Ebola.Vile vile hakuna taarifa ya mtu mwingine
yeyote kwenye familia hiyo au kwenye maeneo ya kijiji hicho au cha jirani kuwa
na dalili za ugonjwa huo.
Kufuatia taarifa hii, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa
kushirikiana na Mkoa wa Kagera imechukua hatua zifuatazo;
• Imepeleka timu ya wataalamu mbali mbali kutoka Wizarani na
mkoa kwa lengo la kwenda kufuatilia na
kutoa taarifa kuhusu kuwepo kwa ugonjwa huo.
• Imetoa elimu ya Afya kuhusu njia za kuzuia kuenea ugonjwa
wa Ebola pamoja na dalili za ugonjwa
huu, kwa wananchi na watumishi wa afya katika hospitali ya Nyakahanga
• Kupeleka vifaa kinga katika hospitali ya Nyakahanga pamoja
na maeneo ya mipakani
• Kutoa matangazo kwa jamii kwa kutumia vipaaza sauti na
kupitia radioni (Radio Karagwe) kuhusu
ugonjwa huu. Aidha, vipeperushi pia
vimetolewa.
Hitimisho
Wizara inapenda kuufahamisha umma kuwa mpaka sasa hakuna
mgonjwa yeyote aliyethibitishwa kuwa na ugonjwa wa Ebola hapa nchini.Aidha,
Wizara ya Afya imejiaanda kikamilifu kukabiliana na ugonjwa huu iwapo utatokea
hapa nchini.
Kwa sasa timu za wataalum
zipo katika mikoa ya Mara, Mwanza, Kagera, Kigoma, Kilimanjaro na
Arusha, kutoa elimu juu ya ugonjwa huu kwa wataalamu na kwa wananchi na
vilevile kufuatilia ugonjwa huu sehemu za mipakani.
Wizara inaendelea kutoa wito kwa wananchi kutoa taarifa
haraka kwenye kituo chochote cha kutolea huduma za afya, mara wanapoona dalili
za ugonjwa huu.
Imetolewa na:
kitengo cha
Mawasiliano
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii
Tarehe 6 Agosti, 2012.