POTISKUM, NIGERIA
Mamia ya wakazi wa mji wa kaskazini mwa Nigeria wa Potiskum wameyakimbia makazi yao wakihofia usalama wa maisha yao kutokana na hofu ya kundi la Boko Haram kufanya tena mashambulio dhidi ya mji huo.
Serikali ya Nigeria imeimarisha usalama katika mji huo baada ya kundi la Boko Haram kufanya mashambulio katika eneo hilo la kaskazini, ambapo watu 30 wanaripotiwa kuuawa.
Hali hiyo imewafanya raia wengi kuukimbia mji huo. Vikosi vya usalama vya Nigeria vinaonekana vikipiga doria na kurandaranda katika mitaa na barabara za mji huo. Aidha baadhi ya raia wanafadhilisha kubakia ndani na hawatoki nje wakihofia usalama wao.
Juzi jeshi la Nigeria lilimkamata mwanachama wa ngazi za juu wa kundi la Boko Haram ndani ya nyumba ya mjumbe wa Baraza la Kitaifa la Senate katika mji wa Maiduguri kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.
Kundi la Boko Haram lilianza kuzishambulia taasisi za kiserikali, kama vile magereza, vituo vya polisi na shule katika eneo la kaskazini mashariki mwa Nigeria tokea mwaka 2009, na hadi sasa limeshaua zaidi ya watu 1,500