SERIKALI imeanza maandalizi ya ujenzi wa barabara ya Dar es
Salaam – Chalinze inayojengwa kwa njia sita, na katika mwaka wa fedha
2013/2014, imetenga Sh bilioni 100 kwa ajili ya kazi hiyo. Waziri wa Ujenzi, Dk
John Magufuli akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara
yake kwa mwaka wa fedha 2013/2014 juzi, alisema barabara hiyo itajengwa kwa
ubia kati ya Serikali na kampuni binafsi.
“Kutokana na tangazo lililotolewa na Wizara kupitia
Tanroads, kampuni 19 zimewasilisha mapendekezo ya jinsi ya kujenga barabara hii
kwa njia sita kuanzia Dar es Salaam – Mlandizi na njia nne kuanzia Mlandizi –
Chalinze.
Akizungumzia barabara kwa ujumla, alisema katika mwaka
2012/2013, Wizara kupitia Wakala wa Barabara (Tanroads), ilipanga kukamilisha
ujenzi wa barabara kuu zenye urefu wa kilometa 414 kwa kiwango cha lami,
kukarabati kilometa 135 kwa kiwango cha lami pamoja na kujenga na kukarabati
madaraja 11.
“Hadi kufikia Aprili 2013, ujenzi wa kilometa 374.65 za
barabara kuu kwa kiwango cha lami na ukarabati wa kilometa 140.63 kwa kiwango
cha lami ulikamilika,” alisema Dk Magufuli. Kuhusu matengenezo ya barabara kuu,
alisema lengo lilikuwa ni kuzifanyia matengenezo kilometa 10,534.3 na madaraja
1,154.
“Hadi kufikia Aprili, 2013, kilometa 6,052.8 za barabara kuu
na madaraja 652 yalifanyiwa matengenezo,” alisema.
Waziri Wa Ujenzi, JOHN POMBE MAGUFULI |
Wakati huo huo, wabunge wameipongeza Serikali kwa kutekeleza
miradi ya ujenzi wa barabara kote nchini kwa ufanisi mkubwa. Mbunge wa Bariadi
Mashariki, Andrew Chenge (CCM), aliitaka wizara hiyo kusonga mbele na kukaza
buti kwa kuwa kazi yao nzuri inaonekana.
Naye Mbunge wa Kasulu Vijijini, Agripina Buyogera
(NCCR-Mageuzi), alisema, “Kwa mara ya kwanza leo nawashukuru sana. Naipongeza
Wizara ya Ujenzi kwa kazi nzuri, ila naomba wanisaidie kuweka lami barabara za
Kasulu.”
Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela (CCM),
aliitaka CCM itembee kifua mbele kwa sababu imefanya kazi kubwa katika ujenzi
wa barabara nchini. Kwa upande wake, Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM),
alisema kwa mara ya kwanza anaunga mkono kwa asilimia 100 bajeti, na kuwa watu
wa Ludewa wataendelea kumuombea afya njema Dk Magufuli.
Mbunge wa Kwela, Ignas Malocha (CCM), alisema Tanzania sasa
ina mtandao mkubwa wa barabara za lami, lakini akaomba wananchi walipwe fidia
wanapobomolewa nyumba zao ili kupisha ujenzi. Naye Mbunge wa Ilemela, Highness
Kiwia (Chadema), alimpongeza Dk Magufuli kwa kutenga fedha kwa barabara za
jimboni kwake, huku Mbunge wa Lushoto, Henry Shekifu (CCM), akitaka fidia
mapema kwa wanaobomolewa nyumba zao.
Wabunge wengine waliochangia na kuipongeza bajeti hiyo ya
Wizara ya Ujenzi ni Joshua Nassari (Arumeru Mashariki – Chadema), Ramo Makani
(Tunduru Kaskazini - CCM), Ezekiel Maige (Msalala- CCM), Kaika Telele
(Ngorongoro – CCM), Cynthia Ngoye (Viti Maalumu- CCM) na Jerome Bwanausi
(Lulindi – CCM).
Kwa upande wao, wabunge kutoka mkoani Tabora, licha ya
kuipongeza Serikali kwa kazi nzuri, wameitaka ikamilishe ujenzi wa barabara za
mkoa huo kwa wakati kama zilivyoelezwa katika mikataba kwani kumekuwa na uzorotaji
katika miradi mingi mkoani humo. Mbunge wa Tabora Mjini, Ismail Aden Rage (CCM)
alisema,
“Sina hofu na Kamanda Magufuli, nafahamu wewe unachapa kazi.
Kwa watu wa Tabora, tunakuomba usimamie ili kuhakikisha barabara zetu
zinakamilika kwa wakati.
Nyingi mikataba imeisha na tunadaiwa fidia kubwa.” Mbunge wa
Nzega, Suleiman Zedi (CCM) na Magdalena Sakaya (Viti Maalumu – CCM), waliungana
na Rage kutaka barabara hizo za Tabora zikamilishwe mapema kwa sababu mkoa wao
‘umefungwa’ na mikoa mingine.
Katika hotuba yake, Dk Magufuli alieleza kuhusu utekelezaji
wa miradi mbalimbali ya ujenzi wa barabara za lami nchini kote, ujenzi wa
madaraja na vivuko, na kuliomba Bunge limuidhinishe Sh trilioni 1.226, akachape
kazi mwaka 2013/14.
EmoticonEmoticon