MCHUNGAJI wa Kanisa la Pentecoste Assemblies of God Tanzania
(PAGT) Buseresere, Wilaya ya Chato, Mathayo Kachila (45) amefariki dunia huku
watu wengine 15 wakijeruhiwa kwa mapanga kufuatia vurugu kutokana na mgogoro wa
bucha. Tukio hilo lilitokea jana saa 2:27 asubuhi kwenye Soko la Buseresere
baada ya kundi la wananchi kuvamia bucha iliyokuwa na maandishi ya ‘Bwana Yesu
Asifiwe, Yesu ni Bwana’, kuwataka waliokuwa wakiuza kuifunga hali iliyozusha
vurugu. Kwa mujibu wa mashuhuda wa
tukio hilo, wananchi hao wanaodaiwa kuwa waumini wa Kiislamu
walikuwa wamechukizwa na kufunguliwa kwa bucha hiyo, ndiyo wakachukua uamuzi wa
kwenda kuamuru ifungwe.
Inadaiwa kabla ya kufunguliwa kwa bucha hiyo, Wakristo
walifanya mkutano wa Injili Uwanja wa CCM Katoro na kutangaza kuwa, watachinja
nyama yao na kuiuza kwenye bucha maalumu.
“Tulipata taarifa za kufunguliwa kwa bucha hii na tulipofika
kuwaomba waache kuuza nyama yao, waligoma na kuendelea kuuza, baada ya kuona
hilo wafuasi wa Dini ya Kiislamu walikimbilia msikitini na kuunda kikosi cha
kupambana nao,” alisema Mwenyekiti wa Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata)
Wilaya ya Chato, Yusuf Idd.
Alisema licha ya kuwasihi hawakumsikiliza, waliamua kwenda
kupambana.
Katika vurugu hizo, duka la Idd lilivunjwa na kuporwa simu
na fedha, huku pikipiki mbili ambazo hazijafahamika wamiliki zilichomwa moto.
Katika vurugu hizo nyama ndani ya bucha hiyo ilimwagiwa
maji, ikiwamo kuharibiwa kwa madirisha na milango yake.
Licha ya majeruhi kutajwa kuwa 15, waliotibiwa Kituo cha
Afya Buseresere na kuruhusiwa ni Abdallah Shaaban (25), Abubakar Shaaban (27),
Faruk Shaaban (14), Kassim Almasi (23), Yusuf Shaaban (18), Bilal Hassan na
Abdallah Ibrahim.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Geita, Dk John
Lumona alisema majeruhi wengine waliofikishwa ni Yasin Rajabu (56), Said
Taompangaze (47), Masoud Idd (21), Ramadhan Pastory (36), Haruna Rashid (61) na
Sadiq Yahya (40), ambaye hali yake ameieleza kuwa mbaya na alipelekwa Hospitali
ya Rufani Bugando. Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geira, Paul Katabago
alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuahidi kutoa taarifa rasmi baada ya
kumalizika kwa kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa.
Mkuu wa Wilaya ya Chato, Rodrick Mpogolo aliwataka wananchi
kutulia kwa vile suala hilo linashughulikiwa na serikali na litapatiwa
ufumbuzi.