Dr. Christine Ishengoma |
Na Edwin Moshi.
IRINGA
Mkuu wa mkoa wa Iringa DKT Christine Ishengoma amewataka
wanahabari kulisaidia Taifa katika zoezi la sensa ya watu na makazi kwa
kuendelea kuhamasisha wananchi kujitokeza katika zoezi hilo.
Mkuu huyo wa mkoa ametoa Rai hiyo leo katika ukumbi wa Ruco
mjini Iringa wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku mbili ya wanahabari kutoka
mikoa ya nyanda za juu kusini pamoja na mkoa wa Lindi na Mtwara.
Alisema kuwa zoezi hilo la sensa ya watu na mkazi lina
nafasi kubwa katika Taifa ili kuwezesha kupanga bajeti kulingana na mahitaji
sahihi ya wananchi wake,hivyo kuwataka wanahabari hao kusaidia kutoa elimu
zaidi kwa umma .
Hivyo alisema kuwa ni wajibu kwa wanahabari kuelimishwa
zaidi juu ya zoezi hilo litakavyofanyika Kama njia ya kuwezesha Taifa
kufanikisha zoezi hilo.
Alisema kuwa vyombo vya habari ni miongoni mwa wadau wakubwa
ambavyo vinategemea zaidi Takwimu katika kufikisha ujumbe kwa Taifa hivyo ili
zoezi hilo liweze kufanikiwa lazima kuwepo na ushirikiano mkubwa kutoka kwa
vyombo hivyo vya habari.
DKT Ishengoma alisema kuwa hadi kufikia siku ya zoezi hilo
la sensa ni siku 13 ndizo zilizosalia hivyo ni matumaini ya serikali kuona siku
zilizobaki zinatumika vema katika kufikisha taarifa kwa wananchi.
Alisema kuwa sensa ya watu na makazi ni zoezi ambalo
limekuwa likifanyika kila baada ya miaka 10 hivyo lazima umma kujulishwa ili
kujitokeza kwa wingi katika zoezi Hilo.
Mkuu huyo wa mkoa alishauri wakuu wa kaya kuweka kumbukumbu
sahihi ambazo zitawezeshwa makalani wa sensa kupata taarifa zilizo sahihi
katika kufanikisha zoezi Hilo.
EmoticonEmoticon