KAMPUNI ya Bia Tanzania (TBL), kupitia kinywaji cha Redd’s Original
pamoja na Kamati ya Miss Tanzania, jana wamezindua rasmi shindano hilo sambamba
na kuanza kwa mchakato wa kumpata Miss Tanzania 2014/2015.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Meneja wa kinywaji cha Redd’s
Original, Victoria Kimaro, alisema wana furaha kutangaza udhamini wa mashindano
ya kumsaka mrembo atakayemrithi Happipess Watimanywa.
“Nina imani wote tunakumbuka kuwa mwaka 2012 Redd’s ilisaini mkataba na
Lino International Agency, ambao ndio
wanaoratibu shindano hilo na kuwa wadhamini wakuu wa shindano hili lenye hadhi yake hapa nchini kwa miaka mitatu,
yaani 2012 hadi 2014, hivyo huu ukiwa ndio mwaka wetu wa tatu kwa mujibu wa
mkataba, tunayo furaha kubwa kusema kuwa, Redd’s imeweza kutoa mchango wake kwa
jamii ya Kitanzania, hususan tasnia hii ya urembo,” alisema Kimaro.
Kimaro aliongeza kuwa, wametenga sh milioni 500 zitakazoendesha
shindano hilo katika ngazi zote.
Naye Mkurugenzi wa Lino, Hashim Lundenga, alisema kuwa wao kama
waratibu wakuu wana kila sababu ya kuwashukuru Redd’s Original, kwani zaidi ya
kuwa mdhamini mkuu kwa miaka mitatu,
kinywaji hicho kimekuwa mdau mkubwa wa mashindano haya kwa miaka mingi.
“Kwa niaba ya Lino na wadau wa tasnia ya urembo, tunawapongeza sana
Redd’s Original kwa imani yao kubwa na mashindano haya, ambayo hakika sasa
yanavutia zaidi,” alisema Lundenga.
Aliongeza kuwa wana imani kubwa kuwa mwisho wa mkataba huo wa miaka
mitatu si mwisho wa uhusiano mzuri kati ya Lino International, wadau wa urembo
na kinywaji cha Redd’s Original.
Aidha, Lundenga aliweka wazi ratiba ya mashindano hayo, ambako kuanzia
Aprili hadi Mei ni ngazi ya wilaya na Juni itakuwa mikoa kabla ya kusitishwa
Julai kuupisha mwezi wa Ramadhani.
Baada ya hapo, mashindano yataendelea Agosti katika ngazi za kanda na
shindano la taifa litafanyika Septemba katika tarehe itakayotajwa baadaye.
EmoticonEmoticon