NA Christopher Nyenyembe
WIMBI la wizi wa
fedha kwenye mitandao ya benki kupitia njia ya mashine za kuchukulia fedha
(ATM), umewatia hasara wateja wengi wa benki ambao zaidi ya sh milioni 20
zinadaiwa kuchotwa kwa nyakati tofauti na watu wanne wanaomiliki kadi zipatazo
150.
Uchunguzi uliofanywa na Tanzania Daima Jumatano umegundua
kuwepo kwa mtandao wa wizi kwa njia ya ATM unaotumiwa na watu wanaojifanya kuwa
ni madalali wa fedha wanaowalaghai watumishi wa serikali.
Madalali hao wanadaiwa kuwakopesha watumishi hao wa serikali
kwa sharti kwamba wawapatie kadi zao za kuchukulia fedha benki kama dhamana.
Uchunguzi umebaini kuwa, mtindo huo umeenea katika maeneo
kadhaa mkoani Mbeya na hasa ukiwalenga watumishi wa serikali ambao kutokana na
hali ngumu ya kifedha, wamejikuta wakiingia kwenye mtego huo na kuamua kutoa
kadi zao za ATM ili waweze kupata mikopo.
Habari ambazo gazeti hili imezipata kutoka kwa waathiriwa wa
wizi huo wa mtandao, unasema kuwa wapo madalali ambao wanawafuata watumishi wa
serikali kwa lengo la kuwakopesha fedha kwa masharti kwamba watoe kadi zao za
ATM na namba za siri kama dhamana.
“Mtandao wa kuchukua fedha kutoka kwa watumishi wa umma
umeenea sana, haukuanza leo, wapo watu wanakopesha fedha kwa sharti la kutoa
kadi ya ATM na namba yako ya siri ili mshahara wako unapoingia, wao wanakwenda
kuchukua fedha zao walizokopesha na riba,” alisema mtumishi mmoja wa serikali
jijini Mbeya.
Wakati hali ikiwa hivyo, habari kutoka Wilaya ya Rungwe
zinadai kuwa kiasi kikubwa cha fedha kimechukuliwa benki na watu wanaomiliki
kadi za ATM zaidi ya 120, na kwamba tayari Jeshi la Polisi linawashikilia watu
hao ambao wamekutwa na idadi hiyo ya kadi zisizokuwa zao.
Habari zaidi zinasema kuwa, mtandao wa madalali hao wa fedha
umekuwa mkubwa, na kwamba watu hawaibiwi kwani wametoa kadi zao wenyewe baada
ya kukubali kukopeshwa.
“Ndugu mwandishi tumefikia uamuzi huu kutokana na hali ngumu
ya maisha, watoto wanatakiwa walipiwe ada, tunahitaji mbolea kwa ajili ya
kilimo na gharama za maisha zipo juu, tutafanyaje? Ndiyo maana tumejikuta
tukitoa kadi zetu za ATM ili tutatue matatizo yetu, kama wapo matapeli hilo sijui, ila wengi
tumeingia kwenye mtego huo,” alisema mama mmoja aliyejitaja kuwa ni muuguzi.
Meneja mmoja wa benki ambaye hakutaka jina lake liandikwe
wala benki anayofanyia kazi, alisema wizi kwa njia ya ATM ni tatizo sugu kwa
wateja wao, kwani wamekuwa wakipokea malalamiko kila siku kuwa fedha zao
zinaibwa bila wao kujua.
Alisema hana taarifa kama
kuna wateja wanaotoa namba zao za siri na kadi zao kwa madalali wa fedha.
“Kinachonishangaza benki yetu inakopesha, sasa huu mtindo
uliozuka kati ya wateja na madalali wa nje unatia shaka usalama wa fedha kwenye
benki zetu, inabidi hatua kali zichukuliwe kwa wateja wanaoruhusu watu wengine
wawachukulie fedha, hilo
ni kosa la jinai kufanywa na wateja wasiokuwa waaminifu,” alisema meneja huyo.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya, Diwani Athuman
alipohojiwa alisema kuwa amepokea taarifa za kuwepo kwa tukio hilo, hasa Wilaya
ya Rungwe na kwamba tayari anasubiri taarifa kamili kutoka kwa Mkuu wa
Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Mkoa wa Mbeya (RCO) ili atoe taarifa kamili leo.
EmoticonEmoticon