POLISI wilayani
Rungwe, mkoani Mbeya, limewanasa watu wanne akiwamo mwanafunzi aliyemaliza
kidato cha nne mwaka jana, wilayani Bunda, mkoani Mara, baada ya kukutwa wakiiba
fedha Benki ya NMB tawi la Tukuyu kupitia mashine za kutolea fedha (ATM).
Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Chrispin Meela alisema tukio hilo lilitokea juzi saa
2:30 usiku.
Meela aliwataja watuhumiwa
hao kuwa ni mkazi wa mjini Tukuyu,
Mfanyabishara wa Mbozi, mwanafunzi aliyemaliza kidato cha nne mwaka jana
wilayani Bunda na mkazi wa Msasani Tukuyu.
Alisema akiwa nyumbani kwake usiku, alipigiwa simu na
msamaria mwema na kuambiwa taarifa za kuwapo watu wakiwa kwenye mashine hizo za kutolea fedha,
huku wakiwa wanatoa fedha mfululizo na aliwatilia shaka.
“Jana usiku saa 2:30
nilipigiwa simu na msamaria mwema na kuniambia kuwa, kuna watu wapo Benki ya NMB wanatoa fedha ATM
tena mfululilo huko wakiwa na kadi nyingi za ATM,” alisema Meela na
kuongeza:“Baada ya kuambiwa hivyo nilimpigia simu OCD (Mkuu wa polisi wilaya),
akatuma timu ya makachero eneo ta tukio na wakabahatika kuwakuta na kuwatia
nguvuni.”
Meela alisema watuhumiwa
walikutwa wakiwa na kadi bandia za ATM 150 za watu tofautitofauti na kwamba, hadi wanatiwa mbaroni tayari
walikuwa na Sh20.5 milioni mkononi. Alisema kadi zote ni za NMB na kwamba,
zilikuwa zinaonyesha wateja wote ni
walimu kutoka wilayani Mbozi.
Alisema baada ya watuhumiwa kuhojiwa walidai ni wafanyabiashara wanajihusisha na
kukopesha fedha walimu, hivyo katika
kuzirejea fedha hizo walimu waliwapatia kadi zao ili waende kutoa benki.
“Kinachotupa hofu
hapa ni kwamba, kadi zote hizi zinaonyesha wateja kutoka wilayani Mbozi,
sasa swali kwa nini waje kutolea fedha hizo wilayani kwetu?” alihoji Meela.
Alisema watuhumiwa wote wapo Kituo cha Polisi Tukuyu kwa
mahojiano zaidi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Diwani Athumani alikiri
kupata taarifa hizo, lakini alikataa
kulitolea ufafanuzi kwa sababu
wanaendelea na uchunguzi.
EmoticonEmoticon