MKUU wa Wilaya ya Tarime, John Henjewele, ametoa onyo kwa
baadhi ya walimu wakuu wa shule za sekondari wanaotumia vibaya madaraka na
kuwachangisha michango mipya wananchi bila maelezo ya msingi.
Henjewele ametoa kauli hiyo wakati wa kikao cha Baraza la
Madiwani wa halmashauri ya wilayani hapa juzi.
Alisema kuanzia sasa atawaagiza wakaguzi wa ndani kukagua
hesabu zote katika shule za sekondari wilayani hapa.
Alisema katika siku za hivi karibuni wazazi wamekuwa
wakielezwa kuchangia fedha nyingi kila mwanzo wa muhula wa kwanza wakati hakuna
hesabu maalumu katika shule hizo zinazoonyesha matumizi ya michango ya mwisho
wa kila mwaka.
“Baadhi ya wazazi wamelalamika juu ya utitiri wa michango
hususan katika shule za serikali za kata kila wanapoanza muhula wa kwanza kila
mwaka kiasi cha baadhi yao
kushindwa kuwapeleka watoto wao kuanza kidato cha kwanza kwa wakati.
“Kuanzia sasa nimewaagiza wakaguzi wa hesabu wa ndani wa
halmashauri kufanya ukaguzi katika shule zote za sekondari…na iwapo
itathibitika kuwa ubadhirifu umetokea na kusababisha upotevu wa fedha hatua
stahiki zitachukuliwa,” alisema Henjewele.
Alisema michango hiyo imegeuka neema kwa baadhi ya wakuu wa
shule hizo ambapo sasa baadhi wamekuwa wafanyabiashara huku wakiacha watoto
bila kufundishwa sawasawa na kusababisha kupatikana matokeo yasiyoridhisha
wakati wa mtihani wa kidato cha nne.
EmoticonEmoticon