Na Rodrick Mushi, Moshi
NAIBU Waziri wa
Uchukuzi, Charles Tizeba, amesema amefedheheshwa na kitendo cha uongozi wa
manispaa ya Moshi kutaka kuua uwanja wa ndege wa Moshi kwa kugawa ardhi ya
uwanja kwa baadhi ya watu.
Mbali na hilo
alisema pia kuna mkanganyiko wa mchoro wa uwanja huo wa awali baada ya
kubadilishwa.
Tizeba alisema hayo mjini hapa jana baada ya kufanya ziara
yake kwenye uwanja huo akiwa ameambatana na Mbunge wa Jimbo la Moshi, Philemon
Ndesamburo.
Katika ziara hiyo walizunguka maeneo mbalimbali ya uwanja
huo na kujionea ujenzi uliofanyika ndani ya uwanja huo.
Akizungumza kwenye kikao kilichofanyika ndani ya uwanja huo,
Tizeba alisema kufa kwa uwanja huo kunachangiwa na watu wa Moshi wakiwemo
baadhi ya viongozi wa manispaa.
Kutokana na hali hiyo alimtaka kufika Ofisa Mipango Miji,
Alex Poteka, ambaye alifika muda mfupi huku majibu yake yakionyesha
kutomridhisha naibu waziri huyo.
Awali akitoa malalamiko kwa Waziri Tizeba, meneja wa uwanja
huo wa ndege, Francis Massao, alilalamika kuomba michoro ya awali ya uwanja huo
toka kwa uongozi wa manispaa akiwamo ofisa mipango miji, Poteka, kwa kuandika
barua bila mafanikio.
“Hivi ni wapi au ni uwanja gani wa ndege unaoweza kuongoza ndege
huku kukiwa kuna nyumba imejengwa katikati ya uwanja!?” alisema Massao.
Tizeba alisema kuwa uwanja wa Moshi ni uwanja mkongwe kuliko
yote ila umechoka kutokana na kutofanyiwa ukarabati muda mrefu.
Kwa upande wake, Poteka alijitetea kuwa hana taarifa kamili
juu ya watu waliojenga kwenye eneo hilo
la uwanja.
EmoticonEmoticon