REPIN ROCK CITY

REPIN ROCK CITY

TUMA TRACK YAKO

FAGIO LA MWAKYEMBE: 11 KIKAANGONI TPA TANGA

11:51:00 PM


FAGIO la Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe la kusafisha uozo katika Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) sasa limehamia katika Bandari ya Tanga ambapo jumla ya wafanyakazi 11 wamepewa barua za kujieleza walivitoa wapi vyeti walivyowasilisha kwa mwajiri wao.

Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na Meneja TPA Tanga, Awadhi Massawe  zilisema wafanyakazi hao ni wale waliopata ajira mpya  Septemba mwaka jana na hatua ya kuwaandikia barua imefikiwa baada ya kuwasiliana na Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA) .

Wafanyakazi hao ni wa Idara za Operesheni, Marine na Ulinzi ambao waliajiriwa  mwaka jana baada ya nafasi zao kutangazwa na kufanyiwa usaili.

Wafanyakazi hao waliopewa barua za kujieleza ni 11 kati ya waliofuzu usaili uliosimamiwa na maofisa wa TPA Tanga na baadaye  kuonekana kufanya vizuri kuwashinda waombaji wengine.

“Hapa bandarini sasa hivi hakuna raha kila mtu ana wasiwasi, hawa  vijana walishaajiriwa na kulipwa mishahara, lakini leo wanaambiwa kuwa hawafai, imetushtua sana,”alisema mfanyakazi aliyejitambulisha kwa jina moja la Mariam.

Ilielezwa kuwa barua za kuwataka watoe maelezo ya vyeti vyao zilianza kusambazwa Jumatatu wiki iliyopita na kwamba hivi sasa baadhi yao hawafiki tena kazini kutokana na kuhofia kukamatwa.

Akithibitisha habari hizi, Massawe alisema ni kweli kuna watumishi 11  waliopewa barua za kujieleza juu ya vyeti vya kuhitimu kidato cha nne na sita, lakini bado hawajafukuzwa kazi.

Meneja huyo alisema katika kipindi cha kukamilisha mkataba wa waajiriwa hao, TPA iliwasilisha vyeti vyao kwenye NECTA ili kujua kama ni halali au la, ndipo ikabainika hao 11 vyeti  vyao havikutoka NECTA.

Alisisitiza kuwa wakati wa ubabaishaji katika kutoa ajira TPA sasa umekwisha ili kuleta ufanisi.
 sheria ili kuleta ufanisi na kuondoa malalamiko ambayo yamekuwa  yakijitokeza mara kwa mara.

“Baada ya NECTA kuvikana  vyeti vya waajiriwa hao wapya, polisi wameanza kufanya uchunguzi ili kuwafikisha mahakamani kwa kughushi vyeti,” alisema.

Inasemekana vyeti hivyo vyote bandia vimetengezwa sehemu moja iliyopo jijini Dar es salaam na kwamba ilibainika hivyo baada ya mmoja wa  wafanyakazi hao kubanwa na kuwataja wengine kuwa wote wamechapishiwa na mtu mmoja.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga,Constantine Massawe hakutaka kuelezea juu ya sakata hilo na kusisitiza kuwa atazungumza na  vyombo vya habari mara uchunguzi utakapokamilika.

MWANANCHI

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »

MNADA BANNER