HUDUMA za matibabu na
upasuaji wa moyo zitaanza kupatikana nchini, kutokana na mipango ya Hospitali
ya Taifa ya Muhimbili na ile ya Aga Khan.
Hatua hiyo itawawezesha wagonjwa wa moyo nchini kutopelekwa
kwa wingi nje ya nchi kama ilivyo sasa. Pia itaokoa mamilioni ya fedha ambazo
zimekuwa zikitumika kugharimia tiba hiyo nje ya nchi.
Mkurugenzi wa Huduma za Afya wa Hospitali za Aga Khan
Tanzania, Dk Jaffer Dharsee akiwasilisha taarifa kuhusu ongezeko la magonjwa ya
moyo nchini katika kongamano la wataalamu wa magonjwa hayo alisema, jitihada
kubwa zinafanywa ili kuhakikisha tiba ya moyo inaanza kutolewa nchini.
Alisema Hospitali ya Muhimbili inakusudia kuanza kutoa tiba
hiyo katika kipindi cha miezi miwili ijayo baada ya ujenzi wa taasisi yake
kukamilika, wakati Hospitali ya Aga Khan itaanza kutoa matibabu hayo mwakani.
Kongamano hilo lilifanyika mwishoni mwa wiki iliyopita jijini Dar es Salaam.
Hatua ya kuwapo kwa tiba za moyo nchini, itawezesha gharama
za tiba kupungua kwa asilimia 57.1, ikilinganishwa na gharama za tiba hizo nje
ya nchi.
Dk Dharsee alisema hapa nchini gharama za tiba zitakuwa Dola
za Marekani 1,500 sawa na Sh2.4 milioni tofauti na Dola 3,500 (Sh5.6 milioni)
zinazotumika kumpeleka mgonjwa kwa ajili ya upasuaji nchi za nje kama India.
Alisema gharama hiyo inatokana na kuwapo kwa gharama kubwa
zinazohitajika kuandaa maabara hiyo ambayo ina thamani ya Dola 200 milioni
(Sh320 bilioni) bila kuingiza gharama za wataalamu wa kuiendesha na kuhudumia
wagonjwa.
EmoticonEmoticon