TANZANIA imetajwa
kuwa ni miongoni mwa nchi zinazokabiliwa na tatizo la rushwa ndani ya jeshi.Taasisi ya
Transparency International (TI), ambayo hutafiti masuala ya rushwa duniani
imeitaja Tanzania kwamba jeshi lake lina rushwa kubwa na ndogondogo.
Kwa mujibu wa gazeti dada la The Citizen la jana Jumapili,
uongozi wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) umekanusha vikali taarifa ya
taasisi hiyo.
TI inadai katika taarifa yake kuwa sekta ya ulinzi ya
Tanzania inakabiliwa na tatizo hilo na hiyo ni kutokana na mambo yake
kuendeshwa kwa usiri mkubwa.
“Hakuna kitu kibaya kama la rushwa kwenye jeshi, maana kuna
fedha nyingi inatembea kutokana na ughali wa vifaa vya kijeshi. Bado Serikali
nyingi zinafanya mambo haya kuwa siri na kutoa mwanya kwa rushwa kutembea.
“Fedha inayotumika vibaya kwa masuala ya kijeshi, ingeweza
kutumia vizuri zaidi katika masuala ya maendeleo,” ilisema sehemu ya taarifa
hiyo iliyoandikwa na Mark Pyman, ambaye ni Mkurugenzi wa Kitengo cha masuala ya
Ulinzi cha Transperancy International.
Transparency International inaeleza kuwa fedha ya rushwa
inayotembea kwenye sekta ya ulinzi inakadiriwa kufikia kiasi cha Dola 20
bilioni (Sh32 trilioni).
“Ripoti ya Transparency International itufungue macho
Watanzania maana kwa kawaida huwa kila watu wakihoji mapato na matumizi ya
jeshi tunaambiwa hatuwezi kujibiwa kwa madai ya woga wa kuhatarisha usalama wa
taifa,” alikaririwa mbunge mmoja na gazeti la The Citizen.
Tanzania, hata hivyo, iko juu ya nchi nyingi za Afrika kwa
tatizo la rushwa ingawa inatakiwa kurekebisha mianya mingi kwenye sekta hiyo.
“Tunaona Tanzania ina changamoto ya kuimarisha vyombo vya
kutupa jicho kwenye jeshi. Mathalani, kuna Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Mambo
ya Nje, lakini haina meno ya kuingia kwa undani masuala ya kijeshi,” iliongeza
Transparency International.
Msemaji wa JWTZ, Kanali Kapambala Mgawe, hata hivyo,
alikaririwa na gazeti la The Citizen akidai kuwa taasisi yake imekuwa ikifanya
kazi kitaalamu na kimaadili akitolea mfano jinsi wanavyoajiri wanajeshi kwa
kufuata vigezo.
Transparency International inasema kuwa kuna Kitengo cha
Utawala Bora cha Serikali ambacho hufanya ukaguzi kwenye jeshi ingawa halijatoa
ripoti ya aina yoyote kuhusiana na ukaguzi wa bajeti ya jeshi. “Mfano kuna
taarifa kuwa Kitengo cha Kilimo cha Jeshi la Kujenga Taifa (Suma-JKT) kuna
kinajishughulisha na uchimbaji madini na biashara nyingine lakini kuna udhibiti
mdogo,” iliongeza taarifa yao.
Julai mwaka jana, maofisa saba waandamizi wa Bodi ya Zabuni
ya Suma-JKT walifunguliwa mashitaka ya matumizi mabaya ya ofisi na uhamishaji
usio wa halali wa zaidi ya Sh 3.8 bilioni.
Waliotuhumiwa ni pamoja na Kanali Ayoub Mwakang’ata, Luteni
Kanali Mkohi Kichogo, Luteni Kanali Paul Mayavi, Meja Peter Lushika, Sajini
John Laizer, Meja Yohana Nyuchi na Luteni Kanali Felix Samillan wanaodaiwa
kufanya makosa hayo mwaka 2009.
Tanzania imewekwa katika Kundi D kwenye orodha hiyo ya
Transperancy International ya nchi zinazokabiliwa na kiwango cha juu cha rushwa
na vigezo vinavyoangaliwa ni sekta za siasa, fedha, utumishi wa Kundi la D ni
nchi ambazo zinakabiliwa na kiwango cha juu cha rushwa na katika orodha hiyo
zimo pia nchi za Russia na China.
Hata hivyo, nchi zenye kiwango cha juu cha rushwa ziko
katika Kundi F wakati zile zenye kiwango cha chini cha rushwa ziko Kundi A.
MWANANCHI
EmoticonEmoticon