FREE MEDIA
SIKU moja baada ya Bunge Maalum la Katiba
kupitisha Katiba inayopendekezwa, Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), umegoma
kutambua matokeo ya kura zilizopigwa kupitisha Katiba hiyo.
UKAWA ambao unaundwa na vyama vya Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA), Chama cha Wananchi (CUF), na NCCR-Mageuzi, wamekuwa
wakifanya mashauriano na hatimaye kuueleza umma hatua itakazochukua.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Habari na
Mawasiliano CHADEMA, ilisema kuwa viongozi wa CHADEMA wanaendelea na
mashauriano na wenzao katika UKAWA, kupitia vikao vyao vya ndani.
“Baada ya vikao na mashauriano hayo, viongozi wa
UKAWA watawaeleza Watanzania maana ya uharamia huo na watatoa msimamo
dhidi ya uharamia uliofanywa na Bunge Maalum la Katiba,” ilisema taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Bunge Maalum la
Katiba limetumia njia za kiharamia kupata theluthi mbili ya kura za Zanzibar na
kuwahadaa Watanzania kwamba kura hizo ni halali.
Taarifa hiyo ilisisitiza kuwa, BMK lilikuwa sawa
na Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), na limetumia njia za kiharamia
kupitisha katiba hiyo inayopendekezwa.
Taarifa hiyo, imewataka Watanzania kutambua kuwa
BMK limetangaza mgogoro na mwanya mwingine wa agenda kubwa ya kuwaunganisha
Watanzania kupigania mabadiliko ya kweli dhidi ya maharamia wa
demokrasisa na maoni ya wananchi.
“CHADEMA kama walivyo wenzao kupitia
UKAWA, wanajua kuwa Watanzania katika wingi mkubwa ambao kiu yao ya
Katiba Mpya na bora haijakidhiwa, badala yake wameongezewa uchungu, wana
shauku kubwa kusikia maelezo, ufafanuzi wa uharamia uliofanyika Dodoma
juzi na wasubiri kusikia maelekezo ya hatua itakazochukua,” ilisema taarifa
hiyo.
Katika matokeo yaliyotangazwa juzi, Naibu Katibu
wa Bunge Maalum, Dk. Thomas Kashilillah, alisema Bunge hilo lilikuwa na wajumbe
630, kati yao Wazanzibari ni 219 na kwamba, kati ya hao waliopiga kura ni 154
na ili kupata theluthi mbili ya Zanzibar, zilihitajika kura 146.
Kwa upande wa Bara, Dk. Kashilillah alisema
wajumbe walikuwa 411 lakini waliopiga kura ni 335 na ili kupata theluthi mbili
ilitakiwa kura za wajumbe 274.
Alisema kwa mujibu wa kura zilizopigwa, theluthi
mbili ya Zanzibar ilipatikana kwa ibara zote 289 ambapo ilikuwa ikibadilika
kati ya 146,147 na 148 wakati kwa upande wa Bara theluthi mbili ilikuwa
ikibadilika kuanzia 332, 133 na 134 kutegemeana na ibara.
“Kwa upande wa Zanzibar, wajumbe waliopiga kura
za ndiyo za wazi ni kati ya 106 hadi 108, wajumbe kati ya 7 hadi 8 walipiga
kura za hapana za wazi wakati kura za siri zilikuwa kati ya 38 hadi 40 ambazo
zote zilikuwa za ndiyo isipokuwa moja tu ilikuwa ya hapana katika baadhi ya
ibara,” alisema.
Kwa Bara, kura za ndiyo za wazi zilikuwa kati ya
301 hadi 304, kura ya wazi ya hapana ilikuwa kati ya moja hadi tatu, kura za
siri za ndiyo zilikuwa kati ya 29 hadi 31 wakati kura za siri za hapana
zilikuwa kati ya moja hadi mbili.
EmoticonEmoticon