Na Charles
Ndagulla,MOSHI, Kilimanjaro
JESHI la Polisi nchini limemkamata na
kumfungulia mashitaka ya kijeshi askari wake D.260 PC Godlisen anayetuhumiwa
kumtumikisha vitendo vya ngono mwanafunzi wa kidato cha tatu Sekondari ya
Okaoni Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro.
Habari zilizopatikana kutoka ndani ya jeshi hilo
mjini hapa, zimedai kuwa askari huo alifikishwa juzi kwenye mahakama ya
kijeshi, ambako pia mwanafunzi huyo aliitwa kutoa ushahidi.
Septemba 21 mwaka huu, askari huyo anatuhumiwa
kumfungia mwanafunzi huyo kwenye nyumba ya kulala wageni iitwayo Kuwese mjini
hapa, ambako anadaiwa kufanya naye mapenzi na baadaye kupata ajali ya pikipiki
na mwanafunzi huyo kupata majeraha kadhaa sehemu mbalimbali za mwili.
Mwanafunzi huyo, alikimbizwa Hospitali ya Rufaa
ya KCMC kwa matibabu baada ya kupoteza fahamu, lakini alihamishiwa Hospitali ya
Kibosho licha ya hali yake kuendelea kuwa mbaya kwa kile kilichoelezwa ni
kukwepa macho ya watu wengi.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro,
Koka Moita, alikiri kufunguliwa jalada la uchunguzi juu ya tuhuma hizo na
kwamba, kama itabainika kuwa askari huyo alikwenda kinyume na maadili, hatua za
kinidhamu zitachuliwa dhidi yake.
Kamanda Koka, alitetea hatua ya jeshi hilo
kutochukua hatua mapema kuhusiana na tukio hilo, akidai kuwa askari huyo
alikuwa akiuguza jeraha alilolipata katika ajali hiyo na kwamba, baada ya
kupata nafuu aliagiza uchunguzi uanze haraka.
Pamoja na jeshi hilo kumfungulia mashitaka ya
kijeshi askari huyo, taarifa kutoka kwa mmoja wa wazazi wa mwanafunzi huyo,
zinadai kuna juhudi za maksudi zinafanywa kutaka kukwamisha mashitaka dhidi ya
askari huyo.
EmoticonEmoticon